Na Lucy Ngowi
MBUNGE wa Viti Maalum, Dkt. Neema Majule, amehoji Serikali kuhusu hatua zinazochukuliwa kudhibiti mikopo hatarishi yenye riba kubwa inayotolewa na taasisi zisizo rasmi nchini.
Dkt. Majule aliuliza swali hilo Bungeni jijini Dodoma akitaka kufahamu mikakati ya Serikali ya kulinda wananchi dhidi ya mikopo hiyo inayowaathiri kiuchumi.
“Je, Serikali imechukua hatua gani kudhibiti mikopo hatarishi yenye riba kubwa zinazotolewa na baadhi ya taasisi zisizo rasmi?” alihoji Dkt. Majule.
Akijibu, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, alisema kuwa Serikali, kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imechukua hatua kadhaa za kudhibiti mikopo hiyo.
Alibainisha kuwa hatua hizo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupata mikopo kutoka kwa watoa huduma wenye leseni, kama inavyotakiwa na Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.
Naibu Waziri Luswetula pia alisema kuwa Serikali imewatambua na kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watoa mikopo wasioidhinishwa, huku jumla ya programu 69 za mikopo ya kidigitali zilizokuwa zikitoa mikopo bila leseni zikisitishwa na programu nyingine 126 kufungiwa.
“Pia, Serikali imetoa mwongozo maalum kwa watoa huduma za mikopo ya kidigitali ili kuhakikisha uwazi, uendeshaji wa kimaadili, utoaji wa taarifa kamili kuhusu gharama za mikopo na ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali tayari imeandaa rasimu ya kanuni za kusimamia mikopo ya kidigitali, ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika katika mwaka wa fedha 2026/2027, kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa wakopeshaji wa kidigitali nchini.

