Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: MKUU wa Wilaya Ubungo Mkoani Dar es Salaam, . Lazaro Twange amewapongeza wananchi wa Wilaya hiyo kwa kuwa na ari ya kuanzisha miradi ya maendeleo ikiwemo zahanati katika Mitaa yao kama sehemu ya kuisaidia Serikali kusogeza huduma karibu na wananchi
Twange ametoa pongezi hizo alipofanya ziara ya kutembelea utekelezajia wa miradi ya sekta ya afya ikiwemo zahanati ya Msakuzi iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi kwa gharama ya Sh. Milioni 25, na Manispaa ikiongeza Sh. Mil 25, hivyo kufanya ujenzi huo ulio hatua ya lenta kugharimu Sh. Milioni 50.

“Serikali inawapongeza wananchi wa Msakuzi kwa uzalendo walioonesha wa kuchangia maendeleo na kutambua juhudi hizi Halmashauri imetenga milioni 150 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa zahanati hio ili wananchi waanze kupata huduma ndani ya mwaka wa fedha 2024/2025,” amesema.
Pia ametembelea mradi wa ujenzi wa wodi ya wazazi na upasuaji katika kituo cha afya Makurumula, Mbezi na Mpigimagohe ambapo miradi yote iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2024/2025

Amewapongeza viongozi wa Mitaa, Madiwani na watalaam kwa kuendelea kusimamia vyema miradi ya maendeleo huku akiwasisitiza kusimamia ipasavyo miradi hiyo ili ikiamilike kwa wakati na wananchi waanze kupata huduma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa Dkt. Tulitweni Mwinuka ameshukuru kwa ziara hiyo na kusema usimamizi wa miradi hiyo utakuwa wa karibu kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia wananchi kupata huduma za afya karibu na maeneo yao badala ya kutembea umbali mrefu hasa wamama wajawazito

Wananchi wa maeneo hayo kwa nyakati tofauti wameiomba serikali kusimamia miradi hiyo ikamilike kwa wakati ili waweze kupata huduma katika maeneo yao ya karibu