Na Waandishi Wetu
DARAJA la J.P. Magufuli nchini Tanzania, lililojengwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) ikishirikiana na Kampuni ya China Railway 15th Bureau Group Corporation Limited (CR15), liliunganishwa kwa mafanikio makubwa, Oktoba sita mwaka jana 2024.
Ikiwa ni mradi muhimu wa kitaifa nchini Tanzania, daraja hilo linalopita juu ya Ziwa Victoria na kuunganisha Mkoa wa Mwanza na Geita ndilo daraja la Sita kwa urefu Barani Afrika.
Uwepo wa daraja hilo utapunguza urefu wa safari kutoka saa mbili mpaka dakika 15.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua Daraja hilo jijini Mwanza Mei Mwaka huu 2025, na kwamba daraja hilo ni moja ya miradi mikubwa ya kimkakati ya serikali ya Awamu ya Sita anayoiongoza.
Daraja hilo (Kigongo–Busisi) lenye urefu wa kilomita tatu na barabara unganishi Kilomita 1.66, linaunganisha Barabara Kuu ya Usagara–Sengerema–Geita zenye urefu wa Kilomita 90, upana wake ni mita 28.45 unaojumuisha njia mbili za Magari zenye upana wa mita saba kila upande.
Njia ya maegesho ya dharura mita 2.5 kila upande, njia za watembea kwa miguu mita 2.5 kila upande, eneo la kati linalotenganisha uelekeo tofauti wa barabara mita 2.45, kingo za magari mita 0.5 kila upande,
Na kingo za watembea kwa miguu mita 0.5 kila upande. Na Usanifu wa daraja hilo umetumia teknolojia ya madaraja marefu inayoitwa ‘Extra Dosed Bridge’ ambapo kutakuwa na nguzo kuu tatu.
Wakati wa ujenzi, timu ya mradi ilizingatia kanuni ya ‘ujenzi wa kijani’, ikitafiti na kutumia teknolojia za ujenzi rafiki kwa mazingira ili kupunguza athari kwa ubora wa maji ya Ziwa Victoria na kuhifadhi mazingira.
Daraja la J.P. Magufuli (Kigongo-Busisi)
Daraja la Magufuli limejengwa kwa gharama ya Sh. Bilioni 592.6.
Takwimu zinaonyesha kwamba, kwa ujumla mradi huo umetoa jumla ya ajira 29,211 tangu ulipoanza Februari 25, 2020 mpaka Julai 2024 ambapo asilimia 93.33 sawa na ajira 27,262 ni Wazawa, na hivyo umechochea sana ajira za ndani.
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoani Mwanza, Paschal Ambrose amezitaja faida zitakazopatikana baada ya kukamilika kwa daraja hilo kuwa ni pamoja na kupunguza muda wa kusafiri na uwepo wa uhakika wa usafiri kwa saa 24.
Pia kuondoa msongamano wa magari uliokuwa unatokea kwenye feri.
Kwamba daraja hilo litakuwa kiungo muhimu kwa mkoa wa Mwanza na mikoa inayouzunguka pamoja na nchi jirani, pia daraja hilo litakuwa kivutio muhimu kwa mkoa huo wa Mwanza, tena litatumika kama nembo kwa nchi ya Tanzania.
Daraja hilo ni moja kati ya madaraja makubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati, pia ni alama ya ushirikiano wa China na Tanzania katika kujenga jumuiya ya ngazi ya juu ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja.
Kwamba kukamilika kwa Daraja hilo kutakuza kwa nguvu maendeleo ya kiuchumi ya mikoa ya Mwanza na Geita na kutoa msukumo mkubwa katika kuimarisha ushirikiano kivitendo kati ya China na Tanzania.
Mwandishi Zhou Li, mwalimu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tianjin (TFSU)
Barua pepe: sylvanzhou@foxmail.com
Mwandishi Ning Yi, mwalimu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU).
Barua pepe:02706@shisu.edu.cn