Na Lucy Ngowi
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), imezindua Program mbili kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanawake na wasichana kidijitali.
Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dkt. Amos Nungu amezindua program hizo leo Septemba 10, 2024 mkoani Dar es Salaam.
Dkt. Nungu amesema Program ya kwanza inajulikana kama ‘Future Femtech’ inayowasaidia wanawake wenye kampuni changa au mawazo machanga kwenye teknolojia.

Amesema Program ya pili ijulikanayo kama ‘Kuzatech’ inaangalia mabinti ambao walikuwa shule lakini kwa namna moja au nyingine wakashindwa kuendelea na masomo hivyo wamewapa fursa ya kupata mafunzo kidijitali.
“Sasa hizi Program mbili tunazifanya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo,”amesema.
Nungu amesema Kuzatech wataunganika na Future Femtech ambao baadhi yao ni wahitimu wa vyuo vikuu wenye mawazo ya biashara.
“Sasa ina maana hawa wadogo wanapata fursa ya kuungana na hawa wakubwa,” amesema.
Kwa upande wake Meneja Usimamizi na Uhaulishaji Teknolojia Costech, Dkt. Erasto Mlyuka amesema Program hiyo ya Future Femtech inawalenga wasichana ambao wamekuwa ni waanzilishi wa kampuni changa.
Amesema hupewa msaada wa kitaalam kwa maana ya mafunzo elekezi ya kujengewa uwezo pia kupewa fedha za kuwawezesha kufanya biashara zao.
“Tuna Program nyingine kwa ajili ya wasichana ambao hawakumaliza masomo yao inaitwa Kuzatech inawalenga wasichana wadogo wenye miaka kati ya 15 na 20.
“Lengo ni kuwapa ujuzi na taaluma ya kiteknolojia ili waweze kuja na biashara ambazo zinaweza zikasaidia waweze kumudu maisha yao, na wasaidie jamii.

” Na hii yote tunataka kutengeneza ajira kwa wanawake ili na wenyewe wapate nafasi ya kuchangia kwenye pato la nchi na kuwa na kipato halali,” amesema.
Mbunifu kutoka Arusha, ambaye ni mnufaika wa Future Femtech, Pamela Chogo amesema mafunzo aliyoyapata ni chachu kubwa kwenye ubunifu wa biashara.
Amesema Program hizo ni muhimu kwa sababu zinasaidia kupata elimu ya ujasiriamali.