Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imesaini mkataba na Kampuni ya TIL Construction Limited kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Jengo la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STI) Complex jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu amesema kuwa ujenzi huo ni sehemu ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Dkt. Nungu amesema katika mradi huo COSTECH wametengewa Sh. Bilioni 18 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha menejimenti ya mifumo elimu ya juu katika kuwezesha mageuzi ya elimu kiuchumi pamoja na kuboresha miundo mbinu ya COSTECH.
“Kwa hiyo tunafanya ukarabati hapa jengo la makao makuu Dar es Salaam, tumeshapata mkandarasi, tumeshapata vibali pia tunajenga jengo Dodoma,” amesema.
Amesema kiasi hicho cha fedha Sh. Bilioni 18, jumla ya Sh. Bilioni 8 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la STI Complex na ukarabati wa jengo lililopo.
Amesema ujenzi huo utajengwa kwa miezi 12 ukikamilika makao makuu ya tume hiyo yatakuwa Dodoma.
“Dar es Salaam na Zanzibar zitabaki kuwa ofisi za Kanda. Ujenzi ukikamilika tutanunua vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhakikisha ni usaidizi unaotakiwa kuelekea mageuzi makubwa ya kiuchumi,” amesema.
Amesema wana imani jengo hilo litakamilika ndani ya wakati, “Tutapatikana muda wowote tutakaohitajika kuhakikisha kazi haisimami,”.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TIL, Ding Fubing amesema watafanya jitihada zao zote kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda waliopewa.