“Mfanyakazi atakapochelewa kuwasilisha huo mgogoro ndani ya siku 30 anatakiwa kuomba au kuwasilisha maombi ya kusikilizwa nje ya muda,” amesema.
Amesema kwenye maombi hayo mhusika atatakiwa kuweka taarifa ya maombi itakayoambatana na kiapo, pia kama kuna viambatanisho vingine ikiwa vinaisaidia fomu namba mbili ya kusikilizwa nje ya muda navyo vinawasilishwa.
Pia amesema migogoro mingine yote nje ya uachishwaji wa kazi inapaswa kuwasilishwa ndani ya siku 60 ikiwa ni pamoja na madai ya mishahara na migogoro mingine yoyote ambayo mfanyakazi anaona inahitaji utatuzi wa tume hiyo.
Amesisitiza kuwa, ni muhimu kwa wafanyakazi kuzingatia suala hilo la muda, kwa sababu pamoja na kwamba kuna huo mlango wa kupeleka maombi nje ya muda lakini bado mhusika ana wajibu wa kueleza sababu za msingi kwa nini alichelewa kufungua mgogoro.
“Kuchelewa haijalishi ni muda gani hata kama ni siku moja unatakiwa uielezee ile siku moja umechelewa kwa sababu gani na usipoweza kutoa sababu za msingi pia maombi hayo hayataweza kupokelewa na hivyo mfanyakazi unajikuta unakosa haki zako za msingi haki ambazo ungeweza kuzipata kwa kuwasilisha mgogoro ndani ya wakati.
“Lakini katika kuwasilisha maombi kuna vitu vya kuzingatia pamoja na taarifa ya maombi na hati ya kiapo lakini katika hiyo hati ya kiapo lazima ueleze ulichelewa kwa muda gani kwa maana idadi ya siku lazima uzitaje lakini katika hizo siku ulizozitaja umechelewa kwa sababu gani,” amesema.
Amesema sababu zitakazotolewa lazima zithibitishe kweli kila siku iliyozungumziwa ina sababu ya msingi ambayo itasikilizwa na tume.
“Kwa hiyo msisitizo ni kwamba wafanyakazi wanapaswa kuelewa msingi wa sheria, na sheria haina huruma ni msumeno lazima uizingatie,
“Lazima uitekeleze inavyokutaka ufanye kwa yeyote mwenye kudai haki yake anapaswa kuitafuta kwa wakati , usipoitafuta hakuna atakayekuletea haki yako nyumbani,”amesema.