Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Ujenzi wa Mawasiliano ya China (CCCC), Tawi la Tanzania imeungana na watanzania kusheherekea Tamasha la Kati ya Mwezi, la Jadi lenye historia mkoani Dar es Salaam.
Meneja Msaidizi wa CCCC Li Hong Yin amesema hayo katika sherehe hizo zilizoshirikisha raia wa kichina, viongozi wa serikali, wananchi na watoto zilizoadhimishwa katika ofisi zao zilizopo eneo la Kawe Dar es Salaam.

Amesema lengo la tamasha hilo ni kukuza uhusiano wa kitamaduni, kusherehekea mshikamano na kuendeleza ushirikiano wa maendeleo.
“Tamasha hili linaashiria mshikamano wa familia, matumaini na baraka.Tamasha hili si tu ni kusherehekea mila za Kichina, bali ni nafasi ya kuimarisha urafiki wetu na Watanzania,” amesema.
Katika kusherehekea, washiriki walitengeneza keki za mwezi na kufurahia maonesho ya taa za jadi mambo ambayo ni sehemu muhimu ya tamasha hilo.

Pia hafla hiyo iliambatana na mazungumzo kuhusu mchango wa China katika miradi ya miundombinu nchini Tanzania.
Amesema ujenzi wa barabara na madaraja nchini unaofanywa na kampuni hiyo unaimarisha uhusiano kati ya China na Tanzania, si kwa maendeleo pekee bali pia kwa kujenga daraja la urafiki wa kudumu.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mzimuni Kawe, Raia Nassoro ameshukuru kampuni hiyo ambayo mara zote imekuwa ikishirikiana na serikali pindi inapohitajika kufanya hivyo.

“Nimefurahi kushiriki kwenye sherehe hii ambayo inaongeza upendo na urafiki baina ya nchi hizi mbili,” amesema.
Vile vile Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Kawe, Asteria Chuluma amefurahi baadhi ya watoto wa shule hiyo kushiriki katika sherehe hiyo ambayo imewawezesha kucheza michezo mbali mbali, kupewa zawadi na kushiriki chakula cha pamoja.

“Katika sherehe hizi tunajifunza upendo, ushirikiano na umoja. Mnapokuwa na shughuli kama hii wanafunzi wanakuza vipaji vyao kupitia michezo na taaluma,” amesema.