Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: TAWI la Tanzania la Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC), limetoa ripoti ya utafiti ya Ulinganisho kati ya viwango vya China na Ulaya katika usanifu wa ujenzi wa miundo ya chuma hapa nchini.
Katika utafiti huo, umebaini kuwa China inaongoza katika sekta ya miundombinu na ujenzi hapa nchini, huku Uingereza ikiongoza katika eneo la usanifu,upimaji na utekelezaji wa vifaa vya ujenzi, mifumo na michakato.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CCCC leo Disemba 31, 2024 inaonyesha kuwa, ripoti hiyo ya Maendeleo Endelevu ni ya kwanza kutolewa na kampuni hiyo tokea ilipoingia katika soko la Tanzania.
“Ripoti ya Utafiti inaangazia zaidi uchunguzi mkuu wa tawi katika uwanja wa uvumbuzi wa kiteknolojia na ushirikiano wa kimataifa,” imesema.
Taarifa imesema, ulinganisho wa kina wa viwango hivyo viwili ni muhimu ili kuelewa mfanano na tofauti zao na maeneo yanayowezekana ya uratibu na ushirikiano.
Taarifa imeeleza kuwa tawi hilo la CCCC hapa nchini, pamoja na watafiti kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), walifanya utafiti wa kina juu ya tofauti kati ya viwango vya Uchina na viwango vya Uingereza katika vipimo vya miundo, mifumo ya udhibiti, kanuni za muundo na ujenzi kupitia Mradi wa Usafiri wa Mwendo Kasi (BRT), Dar es Salaam.
“Hitimisho la utafiti linaonyesha kuwa muundo ulioundwa kwa mujibu wa miongozo ya kiwango cha Kichina ina uwezo wa kutosha wa kuhimili mizigo inayotumika,” imesema taarifa hiyo.
Lengo la utafiti huo ni kuonyesha uzoefu muhimu katika kutekeleza miradi ya baadaye ya kampuni hiyo ya kichina tawi la Tanzania.
“Tawi litachunguza zaidi njia ya ujumuishaji wa viwango vya China na Uingereza na kuimarisha ushirikiano katika nyanja ya viwango vya sekta ya ujenzi Tanzania.
“Ushirikiano huu hautaboresha tu kiwango cha kiufundi na uendelevu wa mradi, lakini pia kutoa uzoefu zaidi wa vitendo na mawazo ya ubunifu kwa ushirikiano wa kimataifa wa uhandisi chini ya mfumo wa mpango katika kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kimataifa kusonga hadi juu ya viwango,”.
Taarifa imesema CCCC tawi la Tanzania itaendelea kutekeleza kanuni zinazotakiwa za ujenzi, kuimarisha ujenzi, kujitangaza kimataifa kwa viwango vya nchi yao kupitia uvumbuzi wa kiteknolojia pamoja na kkubadilishana uzoefu.
Katika hatua nyingine taarifa hiyo imeeleza kampuni hiyo itatekeleza majukumu yake ya kijamii kwa kuzingatia maisha na ustawi wa watu, ili kuleta manufaa kwa Tanzania.