– Ashauri TANROADS Kutengeneza Maeneo Ya Biashara Saa 24 Ubungo
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameshauri Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam kutengeneza maeneo machache pembezoni mwa Barabara ya Morogoro kwa ajili ya kufanya biashara saa 24.

Chalamila amesema hayo katika ziara yake kwa Wilaya ya Ubungo alipokuwa akikagua Mradi wa Kuimarisha Usalama Barabarani uliopo katika mfumo wa mabasi yaendayo haraka.
Amesema, ni vema TANROADS ikaona umuhimu huo wa kutenga eneo kwa ajili ya biashara saa 24 kwa kuwa barabara hiyo ni kubwa magari mengi hupita.

Amesema hivi sasa Mkoa wa Dar es Salaam umeanza kufanya biashara saa 24 katika eneo la Karume hadi Kariakoo.
Kuhusu mradi huo wa kuimarisha usalama barabarani amesema kumekuwepo na malalamiko toka kwa wananchi kuhusu huduma ya mabasi yaendayo kasi, hivyo serikali inatatua changamoto hizo.
” Huu mradi ni miongoni mwa miradi mipya nchini. Ndii maana haujaenda jiji lingine. Uendeshaji umeonyesha kuna baadhi ya changamoto. Serikali inapitia sera, sheria ili itakapoingiza mabasi mapya changamoto zisiwepo.
“Lengo ni kuwa na watoa huduma zaidi ya mmoja iwe ni ushindani. Serikali haijasinzia inafanyia kazi changamoto nyingi za kisheria, wafanyakazi na nyinginezo za mradi huu ” amesema.
Mhandisi kutoka TANROAD, Beatrice Rweyemamu amesema mradi huo umeanza Novema 2023 kutoka Ubungo hadi Kimara, unatarajiwa kuisha Aprili 30, mwaka huu.
Amesema kumekuwepo na malalamiko mengi kutokana na foleni. Kwani kabla mradi huo haujaanza barabara hiyo ilikuwa na njia nyingi za pembeni, sasa sasa zinatumika njia moja.