Na Lucy Ngowi
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limevitaka vyombo vidogo vya majini kuzingatia usalama wa abiria kwa kuwa na vifaa vya uokozi ndani ya chombo.
Pia imevitaka vyombo hivyo kutosafiri usiku, ikiwa ni pamoja na wamiliki wa vyombo vya uvuvi kujiepusha na tamaa ya kubeba abiria kinyume cha sheria na taratibu kunakosababisha kuhatarisha maisha ya watu.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, imeeleza hayo baada ya kupokea taarifa ya kuzama kwa boti ya MV. Marwa KISS Ziwa Victoria
Taarifa hiyo imesema boti hiyo ilitokea Mwalo wa Iramva kuelekea Mwalo wa Igundu, Wilaya ya Bunda Mkoani Mara Septemba 15, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Taarifa hiyo boti iliyozama ilikuwa imekodishwa kubeba abiria wanaokadiriwa 21.
Imesema kutokana na ajali hiyo abiria 14 waliokolewa, kati ya hao 10 wanaume waliobaki wanawake.
“Hadi kufikia saa mbili usiku Septemba 16, abiria saba walikuwa hawajapatikana , na mwili wa abiria mmoja wa jinsia ya kike ulipatikana,”imesema.
Imesema ufuatiliaji na uokozi wa miili hiyo bado unaendelea.