Na Lucy Ngowi
GEITA: KATIBU wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Ahmed Said, amesema kuwa elimu juu ya uwekezaji na masuala mbalimbali ya kifedha inaendelea kutolewa kwa wananchi kupitia banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika maonesho ya nane ya kimataifa ya sekta ya madini yanayoendelea mkoani Geita.
Akizungumza wakati wa ziara yake kwenye banda hilo, Zena amesema elimu hiyo ni muhimu hasa kwa wananchi ambao wanamiliki fedha lakini hawajui namna ya kuzitumia kwa tija.
“Kuna watu wana fedha nyingi lakini hawajui jinsi ya kuwekeza. Hapa wanapewa maarifa ya kuwekeza kwenye dhamana za Serikali, ambazo ni salama na zenye faida,” amesema Zena.

Katika banda la BoT, wananchi wamekuwa wakifundishwa namna ya kutumia fedha zao kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na uwekezaji kwenye dhamana za Serikali na njia za kujiepusha na utakatishaji wa fedha, jambo alilosema lina athari kubwa kwa uchumi wa taifa.
Amesema elimu hii ni ya msingi kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla, hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inahamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli rasmi za kiuchumi.
Maonesho hayo, yanayofanyika katika Mkoa wa Geita, yamewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wachimbaji, wajasiriamali kutoka Tanzania Bara na Visiwani, pamoja na washiriki kutoka nje ya nchi.

Zena amesema ameridhishwa na maandalizi na ushirikiano uliopo baina ya sekta binafsi na taasisi za umma, akisisitiza kuwa maonesho hayo yanatoa fursa ya kipekee kwa wananchi kupanua uelewa wao kuhusu masuala ya fedha, uchumi na uwekezaji.