Na Lucy Ngowi, Dodoma
DODOMA: BALOZI wa Tanzania nchini Italy, Mbarouk Nassor Mbarouk, ametembelea banda la Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, na kuonesha kufurahishwa na ubunifu na kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo.
Katika ziara hiyo, Balozi Mbarouk amesema amepata “exposure nzuri” juu ya majukumu na shughuli muhimu zinazotekelezwa na TPHPA, hasa katika kuhakikisha usalama wa mazao ya kilimo nchini na kutangaza bidhaa za wakulima wa Tanzania kwenye masoko ya kimataifa.
“Nimejifunza mengi kuhusu namna TPHPA inavyolinda afya ya mimea yetu, na pia kusaidia wakulima wetu kufungua masoko nje ya nchi. Hii ni kazi ya msingi katika maendeleo ya sekta ya kilimo,” amesema.
Awali, Meneja wa Sehemu ya Usimamizi wa Afya ya Mimea na Karantini, Musa Chidinda, alimueleza balozi kuwa hakuna mimea au mazao yabkilimo linaloruhusiwa kuingia nchini au kuuzwa sokoni bila kupitia hatua za uchunguzi, ukaguzi na kupewa vibali vya TPHPA.
“Mkulima yeyote anayetaka kuingiza au kuuza nje mazao yake lazima afuate taratibu za nchi. Tunadhibiti visumbufu vya mimea kuanzia shambani hadi kwenye mipaka yetu, kuhakikisha bidhaa zetu ni salama na zinakidhi viwango vya masoko ya kimataifa,” amesema Chidinda.
Katika mafanikio yanayoendelea kupatikana kupitia TPHPA, Chidinda ametaja kuwa mamlaka hiyo tayari imefanikiwa kufungua soko la parachichi, jambo ambalo limewapa fursa wakulima kuuza zao hilo nje ya nchi.
“Kwa sasa soko la parachichi limefunguliwa rasmi, na mchakato huu unahusisha ukaguzi wa zao hilo tangu lipo shambani hadi linapopelekwa sokoni. Tunahakikisha mkulima anapokea cheti ya usafi na mazao yake yanaingia sokoni kwa kufuata viwango vya ubora vilivyowekwa,” amesema..
Kwa ujumla, ushiriki wa TPHPA katika maonesho ya mwaka huu umeonesha wazi umuhimu wake katika kulinda afya ya mimea, kuzuia visumbufu vinavyoweza kuathiri kilimo, na kusaidia wakulima kufikia masoko mapya ya kimataifa.