Na Danson Kaijage
DODOMA: WAKAZI wa Mkoa wa Arusha wanaohudumiwa na Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Arusha(AUWSA) watanufaika na utumiaji wa maji taka yaliyotibiwa kwa ajili ya matumizi ya kilimo cha umwagiliaji.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA), Justine Rujomba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa ofisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema katika Jiji la Arusha ni kati ya majiji yenye mabwawa makubwa 18 ya kuhifadhi maji taka na maji hayo kugeuzwa kuwa fursa kwa kutibiwa na kubadilishiwa matumizi ya kutumiwa katika kilimo.

Akizungumzia mafanikio Mkurugenzi huyo amesema kuwa kwa sasa Jiji la Arusha halina shida ya maji kwani kila kiunga cha Jiji hilo kinapata maji na zaidi ya maji yanapatikana hata mipakani.
Pia amesema kumekwepo na ongezeko la wateja kutoka 6,262 hadi 10,892 ambao wanapata maji safi na salama na hakuna tatizo la maji tena Jiji laArusha.

Katika hatua nyingine Mamlaka imefanikiwa kufunga dira za maji 360 za lipa kabla ya kutumia ambazo zitasaidia kupunguza malimbikizo ya madeni na malalamiko ya ubambikizwaji wa bili za maji.