Na Lucy Ngowi
MBEYA: MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imesema ushiriki wa VETA katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana ni fursa muhimu ya kuonesha namna taasisi hiyo inavyowawezesha vijana kupitia mafunzo ya ufundi stadi yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore amesema hayo alipotembelea banda la VETA katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayoenda sambamba na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Kasore amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo vijana kugundua vipaji vyao na kuvitumia kwa maendeleo yao na ya jamii.

Katika maonyesho hayo, VETA imeonyesha bidhaa mbalimbali za ubunifu kutoka kwa wanafunzi na wakufunzi wake, zikiwemo kazi za watu wenye mahitaji maalum kama ishara ya matokeo chanya ya elimu jumuishi inayotolewa na taasisi hiyo.
“Tumekuja na mifano halisi ya bidhaa na bunifu mbalimbali zinazotengenezwa na wanafunzi wetu ili kuonesha matokeo chanya ya mafunzo tunayotoa,” amesema.
Amesema wanawake wengi pia wamenufaika kwa kupata ujuzi wa ziada unaowawezesha kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi, kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji zinazoshirikisha VETA.
Kasore amesema VETA inatekeleza mkakati wa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa lengo la kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa wananchi kupitia programu shirikishi.
Amesema kupitia ushirikiano huo, zaidi ya wanawake 15,000 nchini kote wamepatiwa mafunzo kupitia mpango wa ‘Wanawake na Samia”, uliolenga kuwawezesha kiuchumi na kijamii.
Aidha, amewahimiza wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum kuwapeleka katika vyuo vya VETA badala ya kuwaficha majumbani, akisema taasisi hiyo ina miundombinu na walimu waliobobea katika kutoa mafunzo kwa makundi hayo.
Kasore amesema VETA ni taasisi pekee nchini yenye mamlaka ya kuandaa mitaala ya mafunzo ya ufundi stadi, hivyo kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanalingana na mahitaji ya soko na mabadiliko ya teknolojia kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa.