Na Mussa Juma
ARUSHA: SERIKALI za Afrika Mashariki zimetakiwa kuondoa vikwazo vinavyoathiri biashara ya mipakani ya mazao ya kilimo ikolojia (Kilimo Hai), ili kuwawezesha wajasiriamali wadogo kunufaika na fursa hiyo.
Utafiti kuhusu biashara ya kilimo ikolojia mipakani umebaini changamoto mbalimbali kama viwango vya ubora wa bidhaa, mifumo ya kodi, vikwazo visivyo rasmi barabarani, udhibiti hafifu wa bidhaa zisizo na ubora, na uelewa mdogo wa wajasiriamali kuhusu taratibu za biashara ya mipakani.

Akisoma mapendekezo ya kisera kutoka warsha ya wadau, Ofisa Utetezi na Ushawishi wa Shirikisho la Wakulima Tanzania (SHIWAKUTA), Thomas Laizer, amesema ni muhimu kuchukua hatua madhubuti kuondoa au kupunguza vikwazo visivyo vya kikodi (NTBs), ikiwemo mazuio yasiyo rasmi ambayo huathiri biashara hiyo kwa kiasi kikubwa.
Laizer ameongeza kuwa vikwazo hivyo vinavuruga mfumo wa biashara na kuwaumiza wakulima, kwani wafanyabiashara hulazimika kununua mazao kwa bei ya chini ili kufidia hasara wanazotarajia kukumbana nazo wakati wa usafirishaji.

“Hali hii huwachochea baadhi ya wafanyabiashara na wazalishaji kutumia njia zisizo rasmi kusafirisha bidhaa, jambo linalosababisha serikali kukosa mapato muhimu ya maendeleo,” amesema Laizer.
Amesema pia kuwa serikali na wadau wanapaswa kuwekeza katika elimu kwa wakulima kuhusu mahitaji ya kisera na kisheria ya uzalishaji wa mazao ya kilimo ikolojia, ili waweze kushiriki ipasavyo katika biashara ya mipakani na kukuza uchumi wa kilimo endelevu.
Aidha, amehimiza serikali kuboresha miundombinu, sera rafiki na mikakati shirikishi itakayowawezesha Watanzania kufikia masoko ya kimataifa kwa bidhaa ghafi na zilizoongezwa thamani, hivyo kuongeza mapato ya taifa.
“Tunatambua kuwa uwepo wa wanunuzi wa nje ni fursa kwa wazalishaji wadogo. Serikali inapaswa kuhakikisha mazingira ya biashara ni wezeshi na ya uwazi, ili walengwa wanufaike, haki izingatiwe, na serikali ipate mapato stahiki,” amesisitiza Laizer.
Pia ameeleza kuwa kuna haja ya kuzijengea uwezo taasisi zinazodhibiti ubora wa mazao kwa kuwapatia rasilimali watu na vifaa, ili kulinda walaji dhidi ya bidhaa hatarishi kwa afya na mazingira.
Kwa mujibu wa Laizer, wamependekeza Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutumia nafasi yake kuhimiza nchi wanachama waweke sera za pamoja zitakazoifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa ukanda wa uzalishaji na biashara ya mazao ya kilimo ikolojia, kwa lengo la kulinda afya, kuhifadhi mazingira, na kuongeza ushindani wa bidhaa za ukanda huu kimataifa.

Akizungumza kuhusu utafiti huo, Ofisa Miradi wa SHIWAKUTA na MVIWAARUSHA, Damian Sulumo, amesema endapo vikwazo vya biashara vitaondolewa, uzalishaji utaongezeka kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara ili waweze kuuza bidhaa zilizosindikwa badala ya malighafi pekee.
Naye mshauri wa biashara za kilimo ikolojia kutoka Shirika la Muungano wa Uhuru wa Chakula Afrika (AFSA), Africa Kiiza, amesema anaamini mapendekezo yaliyotolewa yatafanyiwa kazi. Aliongeza kuwa AFSA itaendelea kuwajengea uwezo wabunge wa EAC, wanahabari, na wafanyabiashara wa sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mratibu wa SHIWAKUTA, Richard Masandika, amesema utafiti huo uliofanyika katika mipaka ya Tanzania na Kenya, Kenya na Rwanda, pamoja na maeneo mengine ya Afrika Mashariki, umeleta mafanikio makubwa.
Amesisitiza kuwa kuna nafasi ya kutumia taratibu za kisheria na kikanda za EAC kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara wa mazao ya kilimo ikolojia.

Warsha hiyo ya siku mbili iliyofanyika jijini Arusha, ilihusisha wakulima, vyama vya wakulima, watafiti na wanahabari kutoka nchi za Afrika ya Mashariki, waliokuwa wakijadili matokeo ya utafiti wa AFSA kuhusu biashara ya kilimo hai mipakani.