Yu Minghong
(Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing, China)
Nchini China, watu husema kwamba vijana wa Gen-Z ndio “wenyeji wa mtandao wa intaneti”.
Wanapenda kurekodi na kuonyesha maisha na fikra zao kwa teknolojia.
Katika Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing (BFSU) nchini China, baadhi ya wanafunzi wanaosoma lugha za Kiafrika wana tabia ya kurekodi maisha yao ya chuo kikuu na fikra zao kwa video fupi.
Kwa kupitia njia hii, vijana hawa wameweza kushirikiana na wenzao wa Afrika katika fani mbalimbali.
Sasa video hizi zimekuwa daraja la kubadilishana na kufundishana kwa staarabu za pande mbili, kukuza uelewano wa kina kati ya vijana, na kuendeleza urafiki na ushirikiano baina ya watu wa China na Afrika.
Ushirikiano kati ya China na Afrika machoni mwa vijana
Katika ushirikiano wa kimataifa, vijana wanachukua hadhi muhimu ya kujenga uelewano na uaminifu kati ya nchi.
Wanafunzi wa Kimadagaska na Kizulu wa BFSU wametengeneza video zenye mvuto mkubwa ziitwazo Mazungumzo ya Kifikra kati ya Vijana wa China na Madagascar na Mazungumzo ya Vijana wa China na Afrika kuhusu Maendeleo ya nchi za Kusini.
Video hizi zimeonyesha jinsi vijana wanavyotafakari nafasi yao katika kuchangia maendeleo ya kimataifa kupitia ushirikiano wa China na Afrika.
Katika muktadha wa Pendekezo la Ustaarabu la Kimataifa, vijana wameshafahamu kwamba ushirikiano wa kisiasa na kijamii unaweza kuimarishwa kwa kuheshimiana na kushirikiana.
Kwa sababu hiyo, wanazingatia kuwasiliana na wenzao wa Afrika moja kwa moja.
Video kama Mazungumzo ya Vijana wa China na Mwalimu wa Zimbabwe Kuhusu Maoni yao juu ya Zimbabwe zinahusu utawala bora, umuhimu wa amani na uadilifu katika maendeleo ya kitaifa, ambazo ni ishara ya kuaminiana kisiasa kati ya vijana wa pande zote mbili.
Utamaduni wa Afrika na China machoni mwa vijana
Kupitia kufundishana kwa tamaduni, vijana wa China na Afrika wanazidi kuelewana kwa undani zaidi.
Wanafunzi wa BFSU hutumia video kuonyesha maisha yao ya kila siku wanaposoma chuoni Beijing na vilevile barani Afrika, pia wameonyesha sherehe na sanaa za kijadi za China na Afrika.
Kwa mfano, wanafunzi wa Kiamhara wametengeneza video kama Sanaa ya Uchezaji Simba wa Kijadi Nchini China, Sikukuu ya Kijadi ya Mwaka Mpya Nchini China, n.k.
Wanafunzi wa Kirundi wametengeneza video kama Kushiriki Kwenye Harusi ya Kijadi nchini Burundi, zote ambazo zimeonesha jinsi wanafunzi wa China wanavyovutiwa na urithi wa mila na desturi za kijadi barani Afrika,
wakatumia video ili kurekodi na kuelezea mila zao za Kichina kwa marafiki wa Afrika.
Vilevile, video kama Kutembelea Ubalozi wa Ethiopia na Kuonja vyakula vya kijadi vya Ethiopia zimeonyesha mvuto mkubwa wa utamaduni wa Kiafrika kwa wanafunzi wa China.
Hii imeonyesha kuwa kujifunza lugha ni zaidi ya kujua matumizi ya maneno na sentensi, bali ni kufahamu historia, utamaduni na hali halisi ya jamii tofauti, na kuheshimiana kwa moyo mweupe.
Hili linadhihirika pia kwenye video kama Sanaa ya Vinyago vya Kiafrika nchini China na Maonyesho ya Sanaa ya Kiafrika kwenye Makumbusho ya Sanaa ya Tsinghua, ambapo wanafunzi walieleza kwa mapana na marefu uzuri wa sanaa ya Kiafrika na jinsi inavyofanana na falsafa ya Kichina.
Aidha, kwenye video kama Methali za Kiswahili na Maana Zake katika Maisha ya Kila Siku, wanafunzi wa kozi ya Kiswahili walifafanua methali mbalimbali na kuzilinganisha na methali za Kichina, wakionyesha jinsi methali hizi zinavyofanana kifalsafa na zinavyoakisi hekima ya kijamii.
Afrika ya leo machoni mwa vijana
Vijana wa China pia wamejaribu kujulisha hali ya Afrika ya leo kwa wengi zaidi kupitia njia mbalimbali.
Kwa mfano, video iliyopigwa na wanafunzi wa Kizulu, Mwalimu wa Afrika Kusini Aelezea Utamaduni wa Nyumbani Kwao na video ya mwanafunzi wa Kiswahili anayesoma shahada ya uzamili,
“Mimi ninasoma Kiswahili nchini Kenya, imejaribu kuvunja dhana potofu na kujenga uelewano wa kweli,”.
Vijana hawa wanatumia fursa hii ili kueleza mitazamo na fikra zao kuhusu mabadiliko ya kijamii.
Aidha, baada ya kwenda kusoma na kuishi barani Afrika na kushuhudia jamii za Afrika kwa macho yao wenyewe, wanafunzi wametumia video fupi, picha na mahojiano, “kama vile Ninavyojifunza lugha za Kiafrika nchini China na Utamaduni wa Kiafrika machoni mwangu,”. wakazipakia kwenye vyombo vya habari mseto na zimeleta simulizi halisi.
Mathalani, mwanafunzi mmoja alieleza mshikamano wa jamii ya Waafrika katika harusi ya kijadi ya Burundi ambayo alihudhuria yeye mwenyewe wakati alipojifunza huko. Video hizi zimekuwa njia ya kuwasiliana na kuelewana kati ya vijana wa Afrika na China.
Zinaweza kuonyesha hali halisi ya jamii, utamaduni, maisha ya watu, n.k.
Sasa, dunia nzima inazidi kukaribiana kupitia teknolojia.
Juhudi za wanafunzi wa BFSU za kutengeneza video fupi kuhusu maisha yao nchini China na barani Afrika, na ndoto zao pamoja na wenzao wa Afrika ni mfano mmoja mzuri katika ushirikiano na mawasiliano baina ya watu wa China na Afrika.
Video hizi si kama rekodi ya maisha tu, bali pia ni daraja la mawasiliano linalozidi kuimarika kupitia lugha, ubunifu, na moyo wa dhati. Kwa ushirikiana na mshikamano, vijana wa Afrika na China wanaweza kujenga jamii yenye mshikamano zaidi, haki zaidi na uelewano wa kweli.
