Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: RAIS mpya wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mwalimu Suleiman Ikomba, ameweka wazi mafanikio aliyoyashuhudia pamoja na viongozi wenzake katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025, wakati akihudumu kama Makamu wa Rais wa chama hicho kikubwa cha wafanyakazi nchini.
Ikomba ameeleza hayo alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa chama hicho.
Pia amesema kwa kipindi hicho walifanikiwa kuimarisha utulivu na mshikamano ndani ya chama, pamoja na kupeleka huduma bora kwa walimu kupitia miradi ya maendeleo ya kijamii.
Amesema nafasi yake ya makamu wa rais ilipatikana baada ya kikao cha chama kuazimia kutangazwa kwa nafasi hiyo, hivyo Uchaguzi mkuu uliofanyika Machi 2023 katika Ukumbi wa Naivera, mkoani Tanga, na kupatiwa dhamana hiyo kupitia kura za wajumbe wa mkutano mkuu.
“Nilikuwa miongoni mwa wagombea wengi waliowania nafasi hiyo, na kwa heshima kubwa, wajumbe walinichagua. Nilitumikia nafasi hiyo kuanzia mwaka 2023 hadi 2025,” amesema Ikomba.
Vile vile Ikomba amesema kuwa moja ya mafanikio makubwa ya uongozi wao ilikuwa ni kurejesha utulivu ndani ya chama, jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa kwa kipindi cha nyuma.
“Tulihakikisha chama kinakuwa na utulivu wa kutosha. Zamani kulikuwa na sintofahamu na migogoro ya mara kwa mara, lakini tumeweza kutuliza hali hiyo kwa kutumia busara, kusikiliza wanachama wetu, na kushughulikia changamoto zao kwa wakati,” amesema.
Kwa upande mwingine amesema, mradi wa ‘Samia Teachers Mobile Clinic’ ni moja ya mafanikio ya kipekee ambayo yanajivuniwa na uongozi wake, Kwa kuwa kupitia mpango huo, changamoto mbalimbali za walimu zilitatuliwa.
“Tumefanikisha ziara ya kitaifa kupitia Samia Teachers Mobile Clinic, nimefika karibu kila mkoa nchini kasoro mikoa mitatu tu. Hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha walimu wanatatuliwa changamoto zao pale walipo,” amesema.
Kwa upande mwingine amesema kwamba, baada ya kupewa jukumu la kuwa Rais wa CWT, kwa kushirikiana na viongozi wenzake pamoja na wanachama, ataendeleza mafanikio hayo.
“Ninaamini katika uongozi wa pamoja. Tumejifunza mengi, tumeona ni nini kinachowezekana tukifanya kazi kwa umoja. Sasa tupo tayari kuijenga CWT imara zaidi, inayosikiliza, inayohudumia, na kulinda haki za walimu wa Tanzania,” amesema.