Na Lucy Lyatuu
WAZIRI wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro amesema kuwa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD),hadi kufikia Juni 30, mwaka huu tayari imetafsiri sheria 300 kutoka kwenye lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili kati ya Sheria 446 ili watanzania waweze kuzielewa.
Imesema kwa sasa inafanya kazi nzuri ya kutafsiri Sheria kutoka katika lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.
Hayo ameyasema katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam 2025, maarufu kama Saba Saba alipotembelea banda la Ofisi hiyo alisema serikali kupitia kwa mwaka imetenga bajeti ya fedha ili kuiwezesha OCPD iwe kufasili sheria 146 zilizobaki.

Amesema ofisi hiyo ni muhimu kwamba ikishindwa kutekeleza majukumu yake hata mahakama itavurugikiwa iwapo itatumia sheria ambazo haziko sahihi.
“Ofisi hii ni muhimu inawaambia sheria sahihi ni hii ya mwaka huu na toleo hili la urakibu la mwaka huu,” ameeleza Waziri Dk. Ndumbaro.
Amesema Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria katika mchakato mzima wa utunzi na urekebu wa sheria bila ofisi hiyo hakuna sheria ambayo inakwenda bungeni kutungwa.
Dk.Ndumbaro ameongeza kuwa bila ofisi hiyo hakuna sheria ambayo inafanyiwa marekebisho bungeni, hakuna sheria ndogo ambayo inatungwa wala kufafanyiwa urekebu hivyo ofisi hii ni muhimu.
Ameongeza kwa sasa ofisi hiyo inafanya kazi nzuri ya kutafsiri Sheria kutoka katika lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.
Waziri huyo amesema Ofisi hiyo ni muhimu katika mustakabali mzima wa kutunga na kuchakataka sheria za nchi.