Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kubadilisha maisha ya Watanzania kupitia utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi, ubunifu na ujasiriamali katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea mkoanii Dar es Salaam.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Antony Kasore amesema mamlaka hiyo inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kuonesha mchango wake mkubwa katika kuwapatia Watanzania ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira na pia kuwawezesha kujiajiri kupitia fani mbalimbali za ufundi.
“Tunachokifanya kama VETA si tu kutoa elimu ya ufundi stadi, bali ni kuhakikisha kila mwanafunzi anayeondoka kwetu amejiandaa kivitendo kuingia kwenye soko la ajira ama kujiajiri.
“Ujuzi huu unawafanya vijana kuwa wabunifu, waaminifu na wachapakazi katika sekta mbalimbali,” amesema.
Katika banda lao la maonesho, VETA wameonesha mafanikio ya mafunzo yao kupitia bidhaa na huduma mbalimbali walizozibuni wanafunzi kwa kushirikiana na wakufunzi wao.
Ametaja miongoni mwa bidhaa hizo ni mashine ndogondogo za kusaidia wakulima na wafugaji, kama vile mashine za kupukuchua mahindi, mashine za kutengeneza chakula cha mifugo, na incubator zinazotumia umeme pamoja na sola kwa ajili ya kutotolesha vifaranga.
Aidha, VETA imetambulisha bidhaa za usafi na urembo zinazotengenezwa na wanafunzi kama sabuni, mafuta ya kujipaka, na bidhaa nyingine za matumizi ya nyumbani.
“Tunataka kila mwanafunzi wetu aweze kubuni bidhaa, kuijaribu, na kuiingiza sokoni. Tumefungua kampuni tanzu ya VETA ili kusaidia usambazaji na uuzaji wa bidhaa hizi,” amesema.
Amesena Mwaka huu 2025 mamlaka hiyo pia imekuja na suluhisho kwa changamoto za nishati safi, kwa kuonesha aina mpya ya majiko rafiki kwa mazingira, yanayotumia teknolojia ya kisasa kuokoa nishati na kupunguza moshi.
Katika kuunga mkono mabadiliko ya sera ya elimu ya mwaka 2023, ambayo inalenga kukuza ujuzi wa vitendo kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari, VETA wametenga eneo maalum kwenye maonesho hayo kwa ajili ya kuwaelimisha watoto wadogo umuhimu wa kupata ujuzi wa mapema.
“Watoto wanajifunza masuala ya ushonaji, urembo na hata useremala. Wengine tayari wanaonesha vipaji vikubwa. Tunataka Watanzania waanze kutambua fursa hizi wakiwa bado wadogo,” amesema.
Amesema kuna baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu ambao wamejiunga na VETA baada ya masomo yao, tayari wameanzisha kampuni zao kutokana na ujuzi waliopata. Hii inaonesha wazi kuwa elimu ya ufundi stadi ni chachu ya maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
Kupitia ushiriki wake katika Sabasaba, VETA imeonesha kuwa mwelekeo wa nchi katika kukuza ujuzi na ujasiriamali unazidi kuimarika. Kwa mujibu wa Kasore, lengo kuu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kujifunza, kubuni na kujiendeleza kiuchumi kupitia ujuzi wa vitendo.