Na Lucy Lyatuu
MHADHIRI mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Kilavo Hassan amebuni mashine kwa mfumo wa ‘ATM’ ambayo mtu anaweza kujihudumia mwenyewe.
Amesema Hiyo inatokana na kuweka urahisi wa ufanyaji wa biashara pasipo uwepo wa watu,ambapo mbinu mpya na rahisi imebuniwa ambayo itafanya biashara kujiendesha kidigitali.
“Mashine hiyo inawezesha watu kujihudumia huku muuzaji akiwa na uwezo wa kufanya hadi biashara nne kupitia mashine moja pekee,”amesema.
Kila amesema mbinu hiyo inaweza kuwa ahueni kwa wauzaji wa vinywaji ikiwemo juisi, bia, maziwa au maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Mashine hiyo ipo katika maonyesho ya 49 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea .
Amesema Kwa sasa mtu atakuwa na uwezo wa kusimika mashine hizi katika maeneo mbalimbali analotaka kufanyia kazi na kuacha watu wajihudumie.
Amesema Mashine hiyo inampa mtu machaguo matatu kwa ajili ya kulipia, ya kwanza ni sarafu, ya pili ni noti na ya tatu ni lipa namba. Lipa namba ni rahisi zaidi kwa sababu unakuwa na uwezo wa kuangalia utendaji sa biashara zako moja ksa moja kupitia eneo alilopo.
Akielezea mashine hiyo inavyofanya kazi amesema, ili mtu aweze kuhudumiwa anatakiwa kuja na chombo chake cha kubebea kinywaji na maelekezo yote huwekwa.
“Tunaweka maelezo kuwa ukilipia kiasi kadhaa utapata ujazo kiasi gani kama ni kileo au kinyeaji baridi, mtu anakuwa anajua anahitaji chombo kikubwa kiasi gani ili aweze kupata ujazo wa bei anayohitaji,” amesema.
Amesema uwepo wa mashine hiyo pia utawezesha uuzaji wa vinywaji kidogokidogo hivyo kumfanya mtu kuwa na uwezo wa kumudu kwa gharama zake.
“Kama ni maziwa ya Sh500, au juisi au Kileo cha Sh500 mtu anaweza kujihudumia. Mashine hii huweza kuuza hadi bidhaa aina nne bila kuchanganyikana kwa sababu kila bidhaa itakuwa na koki yake maalumu ambayo ina maelekezo kuwa ukitaka maji utapata koki hii, maziwa koki hii, pombe koki hii,” amesema.
Amesema ndani yake, hufungwa matanki yenye ujazo kuendana na mahitaji ya mteja lakini yapo ya kuanzia lita 18 na huweza kuongezwa kulingana na mahitaji ya mteja.
“Mtu akihitaji hii bei hubadilika kulingana na mahitaji yake lakini huanzia Sh14 milioni,” amesema huku akisema hadi sasa wameshapokea oda za wateja mbalimbali.
Akizungumzia usalama wa uendeshaji wa biashara hiyo, amesema mtu anaweza kuijengea kibanda cha nondo kama ambavyo inafanywa na wafanyabiashara wenye majokofu yanayokaa nje.