– Kupitia Usimamizi Bora Wa Mazao Na Viuatilifu Unaofanywa Na TPHPA
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: TANZANIA imeendelea kuimarisha nafasi yake katika soko la kimataifa, hususan Jumuiya ya Ulaya (EU), kupitia juhudi za kisayansi na kisheria zinazolenga kudhibiti ubora wa mazao ya kilimo na matumizi ya viuatilifu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo katika banda la mamlaka hiyo lililopo kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Amesema mamlaka hiyo imeshiriki maonyesho hayo ili kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanyabiashara na watunga sera kuhusu shughuli za udhibiti wa afya ya mimea, matumizi salama ya viuatilifu, pamoja na taratibu za kuuza na kuingiza mazao nchini.
Amesema miongoni mwa mafanikio muhimu ni kuruhusiwa kwa mara nyingine kwa mazao ya Tanzania kuingia katika soko la Jumuiya ya Ulaya.
.
” Hii ni baada ya mamlaka hiyo kutekeleza ukaguzi na maandalizi ya kitaalamu kuhakikisha kutokuwepo kwa bakteria aina ya Zairella, ambaye awali aligundulika katika baadhi ya mazao ya bustani na kusababisha masharti makali ya uingizaji bidhaa kutoka Tanzania kwenda EU.
“TPHPA ilifanya uchunguzi wa kina, ikaandaa ripoti na kuiwasilisha EU. Baada ya ukaguzi wao, waliridhika na hatua zilizochukuliwa. Hii ni fursa ya kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya,” amesema.
Kwa mujibu wa Profesa huyo, katika kuhakikisha tija katika uzalishaji, TPHPA imewekeza katika teknolojia za kisasa kama vile matumizi ya drone na akili mnemba kwa ajili ya kufuatilia na kudhibiti magonjwa ya mimea na wadudu waharibifu mashambani.
Amesema serikali imenunua ndege maalum kwa zaidi ya Sh. Bilioni sita kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya mimea kama ndege aina ya kwelea kwelea wanaoharibu mazao ya nafaka, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuongeza uzalishaji wa ndani na kuuza nje ya nchi.
Kwa mujibu wa TPHPA, yeyote anayehitaji kuingia kwenye biashara ya viuatilifu nchini ni lazima apitie mafunzo maalum, kupata cheti na kuzingatia kanuni zilizowekwa ili kuepuka athari kwa walaji na mazingira.
“Biashara ya viuatilifu si jambo la mchezo. Tunazingatia sheria yetu ya Afya ya Mimea na Viuatilifu kuhakikisha kuwa matumizi yanakuwa salama na sahihi,” amesema.
Pia amesema mamlaka hiyo inasimamia benki ya mbegu za asili, ikiwa na zaidi ya aina 10,000, ili kuhifadhi nasaba za mbegu na kusaidia tafiti zitakazowezesha ubunifu wa mbegu bora zenye uwezo wa kustahimili hali mbalimbali za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, TPHPA inahakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuzalisha mazao yanayokidhi viwango vya kimataifa na kuweza kuingia kwenye masoko ya kikanda na kimataifa kwa ushindani mkubwa.
“Kauli ya Rais kwamba Tanzania iandae chakula cha kuilisha dunia ina maana kuwa tuzalishe kwa tija na kuuza nje. Mamlaka yetu ina jukumu muhimu sana katika kufanikisha hili kwa kudhibiti visumbufu vya mazao na kuhakikisha ubora,” amesema.
Ametoa wito kwa wakulima, wafanyabiashara, na watunga sera kutembelea banda la TPHPA ili kupata taarifa muhimu zitakazowasaidia kuboresha uzalishaji, kufanya maamuzi sahihi ya kibiashara, na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika biashara ya kimataifa.