Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WATAFITI kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia Ndaki ya Afya na Sayansi Shirikishi iliyopo Mbeya, wamebuni programu ya simu janja iitwayo ‘Jichunge’, ambayo inalenga kuboresha matumizi ya dawa za kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (PrEP).
Mradi huu unaendeshwa kwa usimamizi wa Dkt. Christopher Mbotwa, Mhadhiri wa Takwimu, Baiolojia na Epidemiolojia chuoni hapo.
Dkt. Mbotwa amesema programu hiyo ni sehemu ya utafiti mpana unaojulikana kama Jaribio la Programu za Simu katika Kuboresha Matumizi ya Dawa za Kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Amesema lengo kuu la utafiti huo ni kuangalia namna teknolojia ya simu inaweza kutumika kuboresha afya ya umma na kusaidia kufikia malengo ya kimataifa ya kutokomeza UKIMWI kama tishio la kiafya kufikia mwaka 2030.
Amesema ingawa dawa za kinga (PrEP) zimeonekana kuwa na ufanisi mkubwa kwa watu walioko kwenye hatari ya kuambukizwa VVU, changamoto kubwa imekuwa ni ufahamu mdogo, kutotumia dawa kwa wakati, na kukosekana kwa ufuatiliaji wa karibu wa kitabibu.
Dkt. Mbotwa amesema, “Watu wengi wanaopewa dawa za kujikinga hushindwa kuzitumia ipasavyo. Wengine hawajui ni lini waache au waanze kuzitumia, wengine hawaelewi madhara au faida zake. Matumizi yasiyo sahihi yanaweza kupunguza kabisa ufanisi wa dawa hizo.”
Amesema Programu ya Jichunge, inayopatikana kwenye simu janja, imetengenezwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Oslo, Norway ina faida nne ambazo ni,
Kumkumbusha mtumiaji muda wa kutumia dawa kwa usahihi kila siku ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa njia rahisi kuhusu dawa hizo, faida, madhara, na namna bora ya kuzitumia.
Vile vile mtumiaji kuweza kuwasiliana moja kwa moja na mtaalamu wa afya kwa maswali au changamoto za kiafya.
Amesema pia Programu hiyo humuunganisha mtumiaji na mtu aliyepitia mafunzo kuhusu dawa hizo, anayetoa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa wanaotumia PrEP.
Amesema kwa ajili ya kuthibitisha ufanisi wa programu hiyo, utafiti ulifanyika katika mikoa miwili ya Dar es Salaam na Tanga ambapo washiriki wa Dar es Salaam walipewa programu ya Jichunge, huku wale wa Tanga waliendelea kutumia PrEP bila msaada wa programu.
Amesema matokeo ya awali yalionyesha kuwa idadi ya watu waliotumia dawa kwa usahihi Dar es Salaam ilikua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na wa Tanga.
“Hii inaashiria kwamba programu ya Jichunge inaongeza ufanisi wa matumizi ya PrEP na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kupunguza maambukizi ya VVU nchini,” amesema.
Kwa mujibu wa Dkt. Mbotwa, mafanikio haya yanatoa picha halisi kuwa ‘teknolojia ya afya ya kidijitali’ inaweza kuwa sehemu muhimu ya mikakati ya kiafya ya taifa, hasa kwa makundi yaliyo hatarini.
Mpango wa kupanua matumizi ya programu hii unatarajiwa kuendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya ndani na nje ya nchi, huku matumaini yakiwa makubwa kwamba, kwa kutumia mbinu kama hizi, Tanzania inaweza kufanikisha lengo la kuwa na jamii isiyo na maambukizi mapya ya VVU ifikapo mwaka 2030.