Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MKUFUNZI kutoka Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), Mkoani Mtwara, Fadhila Kusaga amesema chuo hicho kinawafundisha wanafunzi namna ya kuongeza thamani kwenye bidhaa mbalimbali ikiwemo korosho na zao la mwani.
Kusaga amesema hayo kwenye Banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), katika maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Mkoani Dar es Salaam.

Amesema wanamfundisha mwanafunzi kuanzia hatua ya uandaaji wa korosho kutokana na uhitaji wa wateja, kisha wanaziweka kwenye vifungashio.
“Pia tunamfundisha mwanafunzi aweze kuji brand ili kuingia sokoni vizuri,” amesema.
Amesema wametengeneza siagi ya korosho baada ya kuona sokoni kwa muda kumekuwepo na siagi ya karanga.
“Sasa hivi kuna bidhaa ya siagi ya karanga, nasi tumetengeneza siagi ya korosho,” amesema.
Kwa upande mwingine amesema katika kuendeleza uchumi wa buluu wamechukua mwani na kuusaga kisha wakapata unga ambao ni tibalishe nzuri inayosaidia matatizo ya viungo.
Amesema tibalishe hiyo pia inasaidia ukosefu wa usingizi, inaondoa stress, inatibu moyo pia inaongeza nguvu za kiume.