Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: “TEKNOLOJIA iko juu sasa hivi, yale mambo ya kuchukua tindo na kuanza kugonga tunaachana nayo. Sasa hivi tunatumia kompyuta kubuni bidhaa unayohitaji,”.
Mwalimu wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Shinyanga, Omar Mabula amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Habari hii katika Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Akiwa katika banda la VETA akionesha bidhaa zilizobuniwa kwa kutumia teknolojia, amesema baada ya kubuni kile unachokitaka unaweka kwenye mashinena kutoa bidhaa ile ile iliyobuniwa kwa kutumia kompyuta.
Amesema yeye ni mwalimu wa mashine inayotumia kompyuta katika kufanya kazi yake.
“Ninafanya kazi mbalimbali na bidhaa tofauti kwa sababu malighafi inayotumika ni tofauti tofauti,” amesema.
Amewakaribisha wanafunzi kusoma kozi hiyo inayofundishwa kwa miezi mitatu.