Na Danson Kaijage
DODOMA: SERIKALI imetakiwa kufuatilia kwa ukaribu fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili iendane na thamani halisi ya fedha inayotengwa.
Hayo yamebainishwa na washiriki walioshiriki katika mdahalo ulioandaliwa na mradi wa maendeleo wa Acrionaid, kuangalia namna nchi inavyoweza kuwekeza bila kuongeza fedha za mikopo kutoka mataifa ya nje na kuongeza madeni kwa taifa.
Mmoja wa wakulima wa zao la Zabibu wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, Nuru Said amesema licha ya Serikali kukopa fedha kwa ajili ya maendeleo, bado kuna fedha ambayo haitumiki ipasavyo katika kuleta tija ya mradi lengwa.
Nuru amesema imefikia hatua ukaguzi pekee wa miradi unatumia fedha nyingi kuliko mradi mwenyewe jambo ambalo linasababisha kuongeza deni kubwa la fedha ya mkopo kwani Serikali haipo makini katika kufuatilia thamani halisi fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi husika.
“Mimi ni Mkulima wa zabibu na tulipewa mradi wa kilimo hicho lakini cha kushangaza waliokuja kukagua wanaeleza kutumia lita 60 za mafuta na ilikuwa ijengwe choo cha matundu mawili ya choo lakini limejengwa tundu moja kwa bajeti hiyo hiyo na hakuna ufuatiliaji wowote,” amesema.
Amesema kwa Serikali kutofuatilia matumizi bora ya fedha inayotengwa kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo ni mwendelezo wa kukuza deni la taifa.
Mratibu wa Actionaid kutoka Zanzibar, Bakari Khamis Said amesema wameona ni muafaka kuitisha mkutano kujadili namna yakushauri kufadhili maendeleo kwa kutumia vyanzo vya ndani.
Amesema kumekuwa na changamoto ya uchumi kukua lakini mahitaji ya kimaendeleo katika masuala ya miradi inakua kila siku na inahitajika kutafuta rasimali za kuendana na maendeleo hayo.
Amesema kwa sasa mashirika ya kimarekani yamesitisha misaada imekuwa ikiathiri maendeleo hivyo wanaweza kuhamasisha watanzania kutafuta rasilimali za ndani kwa kuimarisha usimamizi wa kodi na mapato yasiyo ya kodi kuimarisha usimamizi wa mapato.
Hata hivyo ameeleza kuwa kama serikali itaimarisha usimamizi wa matumzi yasiyo ya lazima,kupunguza posho serikalini , kupunguza gharama za safari inaweza kujikuta haijiingizi katika mikopo ya kibenki ambayo ni ya kibiashara zaidi.
Naye Program Meneja wa Mtandao wa Madeni, Boniface Komba amesema kumekuwa na ukuaji wa deni la serikali lakini suala la kukopa halizuiliki.
Hata hivyo amesema kwa sasa ugharamiaji deni umekuwa ni mkubwa na linaweza sababisha athari kwa huduma za kiafya kutokana na kulipa deni kwa dola licha ya deni kuwa ni himilivu.
Ameeleza pamoja na yote, serikali iwe na nidhamu ya fedha katika ukopaji na kusimamia matumizi kwani baadhi ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), imeonyesha kuwepo na mianya ya upotevu wa fedha.
Samwel Mkwata kutoka Policy Forum and Policy amesema ameangalia nchi namna inavyoweza kuwekeza kwenye maendeleo ya nchi.
Amesema kutokana na misaada kuendelea kupungua nchi ya Tanzania inaweza kujiendesha kwa asilimia kubwa kupitia mabadiliko ya kikodi.
Amesema kuwa katika majadiliano ya kuimarisha uchumi wa nchi ya Tanzania wanaishauri serikali kuwekeza zaidi ili mwisho wa siku wasitegemee misaada toka nje.