Na Waandishi Wetu
KATIKA siku za karibuni Kitengo cha Maudhui Mtandaoni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC Online), kilirusha hewani video za mahojiano zikilenga ushirikiano kati ya China na Afrika.
Kwenye mahojiano hayo, Ning Yi ambaye ni mwalimu wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU), ndiye alikuwa anawahoji maofisa wa serikali na wataalamu kutoka Tanzania na Kenya.
Katika video ya Januari 30, mwaka huu 2025 mahojiano yalijikita kuhusu jinsi ya kuelewa Jumuiya ya China na Afrika yenye Mustakabali wa Pamoja.
Dhana ambayo ilipendekezwa na Rais Xi Jinping, inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika.
Ikumbukwe kuwa Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mjini Beijing mwaka jana 2024 ulikuwa na mada iliyohimiza ujenzi wa jumuiya ya ngazi ya juu yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Afrika, inayoendeleza juhudi za kujijenga kuwa za kisasa.
Kwenye mahojiano hayo, Naibu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta, Cavince Otieno Adhere, anaeleza dhana hiyo inasaidia kukuza maendeleo ya kiuchumi ya Afrika na kuimarisha uhusiano kati ya Asia na Afrika.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Omari Juma Kipanga, anaeleza dhana hiyo ni dhihirisho muhimu la ushirikiano kati ya China na Afrika, ikilenga kunufaishana kwa pande zote.
Pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Profesa Daniel Elias Mushi, anasema kwamba nchi za Afrika zimefaidika na FOCAC, lakini ni muhimu kuhakikisha zaidi mfumo wa ushirikiano na kutambua majukumu yao wenyewe.
Cavince Otieno Adhere (kulia), Naibu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta Akihojiwa na Ning Yi, mwalimu wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU)
Pia kwenye video ya Machi 13, mwaka huu 2025, mahojiano yalihusu Matarajio ya Ushirikiano kati ya China na Afrika.
Na kwamba, Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, Iribe Mwangi anaamini kuwa programu za mikopo za China kwa Afrika zimeundwa mahususi na zinastahili kupongezwa.
Mwangi anakanusha kwamba programu hizo ni mtego wa deni na unyakuzi wa rasilimali.
Naye Mwalimu katika Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU), Fredrick Maiso Bosire, anaeleza kwamba nchi za Afrika hazihitaji kuchagua upande kati ya China na Marekani, akitarajia pande zote kuzingatia maendeleo ya watu wa Afrika.
Vile vile wataalamu walijadili suala la unyanyapaa linaloikabili China barani Afrika, ikipendekezwa kuimarisha uwazi wa ushirikiano na kukuza mawasiliano ya kitamaduni, kwamba kunaweza kusaidia kuendeleza ushirikiano wenye amani na manufaa ya pande zote kati ya China na Afrika.
Naye msomi kutoka Tanzania, Dkt. Daniel Ndagala anaeleza katika kitabu chake ‘Utamaduni na Maendeleo Nchini Tanzania’ kuwa utamaduni wa Utani ni falsafa muhimu ya utawala nchini Tanzania.
Falsafa ambayo inaendana na lile lengo la dhana ya jumuiya yenye mustakabali wa pamoja, zote zikilenga kutatua migogoro kati ya makundi, kutetea ushirikiano wa pande nyingi, na kuweka msingi imara wa kukuza maendeleo ya pamoja ya wanadamu.
Hivyo tafsiri ya kina ya utamaduni wa Utani wa Afrika ni muhimu sana kwa kuelewa maana na thamani ya dhana ya jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja.
Mahojiano hayo yote yanatoa mijadala ya kina kuhusu ushirikiano kati ya China na Afrika, yakitoa maoni kutoka kwa wataalamu wa Afrika kuhusu maendeleo ya ushirikiano huo.
Wanasisitiza haja ya pande zote mbili kuimarisha ushirikiano kwa kuzingatia maelewano na heshima za pande zote, na kukuza ujenzi wa Jumuiya ya Kusini mwa Dunia.
Ning Yi, mwalimu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU).
Barua pepe:02706@shisu.edu.cn
Zhou Li, mwalimu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tianjin (TFSU)
Barua pepe: sylvanzhou@foxmail.com