Na Lucy Ngowi
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), inaipokea ndege yake kutoka nchini Marekani itakayotumika kunyunyizia viuatilifu kwa ajili ya uangamizaji wa ndege waharibifu wa nafaka aina ya mpunga, mtama na uwele.
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania kuhusu ujio wa ndege hiyo hapa Tanzania.
Amesema, “Ndege hawa wamekuwa ni wasumbufu sana. Mara nyingi wanavamia skimu za mpunga huko Mbeya Mbarali na maeneo mengine.
“Kwa muda mrefu tunategemea Ndege ya Nzige Wekundu kutoka Nairobi nchini Kenya. Mara nyingine inachelewa na matukio haya yanatokea kwa muda mfupi unakuta skimu 10 zinavamiwa,”.
Amesema ndege inayokuja imenunuliwa kwa Sh. Bilioni sita zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema ndege itakapoanza kazi italeta tija kubwa kwa kuwa uzalishaji utaongezeka, pamoja na masoko.