Na Danson Kaijage
WIZARA ya Kilimo imepanga kukusanya Sh. Bilioni 12.26 kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato.
Shilingi Bilioni 8.66 zitatokana na ukaguzi wa mazao, kodi za majengo na uuzaji wa nyaraka za zabuni, huku Sh. bilioni 3.6 zikipatikana kupitia ada za umwagiliaji na ukodishaji wa mitambo.
Wqziri wa Kilimo, Hussen Bashe ametoa kauli hiyo Bungeni Jijini Dodoma, Wakati akiwasilisha bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara yake huku akiliomba Bunge liidhinishe matumizi ya jumla ya Sh. Trilioni 1.24 kwa mwaka huo wa fedha 2025/26
Waziri Bashe amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imewasilisha mpango wake wa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026,
Amesema mpango huo unalenga kuimarisha ajira staha kwa vijana na wanawake kupitia Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kilimo na miundombinu ya umwagiliaji.
Kuhusu miradi ya Maendeleo na Matumizi ya Kawaida, Wizara imeomba Sh.Bilioni 838.26, ambapo Sh. Bilioni 702.28 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo, zikiwemo Sh. Bilioni 424.33 kutoka vyanzo vya ndani na Sh. Bilioni 277.95 kutoka nje.
Fedha nyingine ni Sh. Bilioni 135.98 zitatumika kwa matumizi ya kawaida, ikiwa ni pamoja na Sh. Bilioni 81.45 kwa mishahara ya watumishi na Sh. Bilioni 54.54 kwa matumizi mengine ya wizara, bodi na taasisi zake.
Waziri Bashe amesema Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaomba kuidhinishiwa Sh. Bilioni 382.14, kati ya hizo Sh. Bilioni 308.72 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo (zikiwemo Shi. Bilioni 259.62 kutoka ndani na Sh. bilioni 49.10 kutoka nje), na Shilingi Bilioni 73.42 kwa matumizi ya kawaida ambapo Sh. Bilioni 8.27 ni kwa ajili ya mishahara na Sh. Bilioni 65.15 kwa matumizi mengineyo.
Kuhusu Tume ya Maendeleo ya Ushirika, jumla ya Sh. Bilioni 22.58 zinaombwa, ambapo Sh. Bilioni 21.88 ni kwa matumizi ya kawaida (mishahara Sh. Bilioni 12.85, matumizi mengineyo Sh. Bilioni 9.03) na Sh. Milioni 697.18 kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa fedha za ndani.
Kwa upande mwingine Waziri huyo mwenye dhamana ya Kilimo amesema Ajira kwa Vijana na Wanawake Kwenye mashamba makubwa mbali na makadirio ya fedha, Serikali imeeleza maendeleo ya utekelezaji wa Programu ya BBT inayolenga kuimarisha ajira za vijana na wanawake kupitia miradi mitano.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mashamba ya pamoja, mitaji, huduma za ugani, uongezaji thamani wa mazao, na umwagiliaji,Shamba la Chinangali (ekari 1,772) limekabidhiwa kwa vijana 261 na linaendelea kuzalisha mazao mbalimbali.