Na Danson Kaijage
DODOMA: SERIKALI imetumia Sh. Bilioni 94.5 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 33 vya ufundi stadi, kati ya hivyo 29 vikiwa vya wilaya na vinne vya mkoa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthony Kasore amesema hayo alipokuwa akielezea mafanikio ya mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuanzia 2021 hadi 2024.
Kasore amesema serikali pia ilitenga Sh. Bilioni 103 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vipya 64 vya Wilaya na kimoja cha Mkoa wa Songwe, ambavyo vitachangia ongezeko la udahili wa wanafunzi 89,700.
Amesema kwa sasa VETA ina vyuo 80 hivyo mwishoni mwa mwaka huu 2025 vyuo vinavyojengwa vinatarajiwa kukamlika na kuwezesha kuwepo kwa vyuo 145 ambavyo vitakuwa mkombozi kwa vijana na watu wazima wanaotarajiwa kustaafu.
Akielezea mafanikio ya Mamlaka hiyo, amesema Serikali kupitia VETA imefanya upanuzi wa miundombinu ya kutolea elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini kwa kutoa fedha ili kuongeza majengo mapya na ukarabati wa majengo ya zamani, kuweka mazingira wezeshi ya kukuza ubora wa mafunzo na kuongeza fursa za udahili katika vyuo vya VETA.
Akizungumzia eneo la upanuzi na uboreshaji wa miundombinu, amesema kipindi cha miaka minne Serikali imetoa kiasi cha Sh. Bilioni 14.2, ambazo zimewezesha uboreshaji na upanuzi wa miundombinu ya vyuo.
Vyuo hivyo ni chuo cha Newala, Ngorongoro, Moshi, Dar es Salaam (Changombe), Kipawa, Mtwara, Mwanza, Mikumi, Karagwe, Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) Kihonda, Nkasi, Nyamidaho, Kanadi, Ileje, Namtumbo, Mabalanga, Gorowa, Arusha na Busokelo.
Kuhusu uongezekaji wa udahili na uhuishaji wa mitaala amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya sita, jumla ya vijana 295,175 wamedahiliwa katika vyuo vya VETA katika kozi za muda mrefu na muda mfupi.
Kuhusu urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo amesema kuwa kupitia Mpango wa Utambuzi na Urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi, katika kipindi cha Mwaka 2021 hadi 2025, jumla ya wanagenzi 5,175 walitambuliwa na kurasimishiwa ujuzi wao.
Amesema kati ya yao wanagenzi 1,164, walikuwa wanaoshiriki miradi ya kimkakati ya Ujenzi wa Reli ya Mwendokasi (SGR) na Bwawa la la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na 214 wapo kwenye vyuo vya kurekebisha tabia ambao ni wafungwa katika Magereza ya Ukonga, Arusha na Morogoro.