Na Lucy Ngowi
Dar es Salaam; TAKWIMU zinaonyesha kuwa mwaka 2019 mpaka Mei mwaka huu 2024 ajali za barabarani zilikuwa zaidi ya 10,000 ambapo idadi ya vifo vilikuwa 7639, majeruhi 12,663.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Zuhura Yunus amesema hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya ustadi wa kuboresha tija ya madereva mkoani Dar es Salaam.
Amesema kati ya ajali hizo asilimia 76 zinasababishwa na makosa ya kibinadamu., pia mawasiliano yasiyoridhisha kati ya madereva na waajiri wao yamesababisha migomo mingi ambayo inaiba muda mwingi wa uzalishaji na kusababisha hasara kwa pande zote mbili.

” Haya yote yanaathiri nguvu kazi ya taifa na yanahitaji kurekebishwa kupitia mafunzo na mbinu nyingine.Hivyo mafunzo haya yamekuja wakati muafaka ili kuweza kuchangia kupunguza changamoto zilizopo ambazo zinaweza kuepukika,” amesema.
Zuhura amesema madereva ni watu muhimu jamii inawategemea kurahisisha uzalishaji na utoaji wa huduma kwa kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine katika harakati za kiuchumi.
“Hivyo hamna budi ninyi madereva kuhakikisha jamii inafanya shughuli hizo za kiuchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema.
