Na Mwandishi Wetu
KIGOMA: WAKUU wa Divisheni na Vitengo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wamepatiwa mafunzo ya utumiaji wa Mfumo wa Kieletroniki yenye lengo la kuongeza ufanisi katika majukumu yao.

Aidha mafunzo hayo ya matumizi ya mfumo huo yataongeza ufanisi wa uandaaji na uendeshaji wa vikao jambo litakalo punguza gharama za maandalizi yake.
Ofisa TEHAMA wa halmashauri hiyo Jamal Sompole ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo ameeleza.
“Mfumo tukiufahamu vyema utasaidia halmashauri kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kuandaa makabrasha kwa kuwa taarifa zote hizo zitakuwa katika mfumo na madiwani na wataalam kuwa na uwezo kuzipakua huko,” amesema.

Naye mwezeshaji mwingine wa mafunzo hayo, Fiona Emmanuel amesema mfumo huo utasaidia kuokoa muda na gharama za kusambaza makabrasha kwa kuwa hivi sasa inawalazimu kuyafikisha katika kata zote 21 zilizopo katika halmashauri.
Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Renaltus Kavishe amesema mfumo huo ukieleweka vizuri utasaidia kurahisisha mawasiliano baina ya watumishi kwa watumishi au watumishi na madiwani kwa kuwa mambo yote muhimu yanayowahusu yapo ndani.

Naye Mkuu wa Idara ya Afya,Lishe na Ustawi wa Jamii wa halmashauri hiyo, Dkt. Chacha Tubeti amesema mfumo huo utasaidiia idara kuwa na uwezo wa kupata taarifa mapema popote mtumiaji atakapokuwa, jambo litakaloboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.