Na Mwandishi Wetu
MAOFISA Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na viongozi wa vyombo vya usalama wa Wizara hiyo, wameagizwa kutekeleza kwa vitendo, pia kuiishi falsafa ya R nne (4R) ya Rais Samia Suluhu Hassan ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza hayo wakati alipofungua Semina elekezi kwa viongozi waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Weruweru River Lodge, mkoani Kilimanjaro
Majaliwa amesema ni muhimu kuifahamu vyema falsafa hiyo ya Rais Samia na kuitekeleza kwa vitendo.
“Nina imani kubwa kwamba uongozi wa juu wa Wizara umeielewa vizuri falsafa hiyo, na semina hii elekezi ni ushahidi tosha wa kuitekeleza kwa vitendo.

“Falsafa hii inajikita katika masuala ya Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga upya Taifa . Hivyo, nitoe wito kwa washiriki ambao ni Maofisa Waandamizi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake kuendelea kushiriki na kuishi kikamilifu falsafa hii,” amesema.
Majaliwa amesema semina elekezi hiyo ni sehemu muhimu kwa maendeleo ya kitaaluma na kitaasisi kwa maofisa waandamizi wa vyombo vya usalama, na husaidia katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kufuata viwango vya kitaaluma na kisheria.
“Semina elekezi hutoa fursa kwa maofisa waandamizi kujifunza mbinu na taratibu mpya katika utendaji wa majukumu yao. Hii inajumuisha teknolojia mpya, mbinu bora za ulinzi na usalama, na mbinu za kisasa za kupambana na uhalifu.” amesema.
Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amemshukuru Rais Samia juu ya nia yake ya dhati kwa kufanya maboresho ya Wizara hiyo na vyombo vyake ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto pamoja na Taasisi ya NIDA.
“Maboresho haya yanahusisha upandishaji vyeo wa kihistoria wa Maofisa, Wakaguzi na Askari wapatao 50,971, kuongeza Bajeti ya Miradi ya Maendeleo kutoka mwaka 2021/22 hadi 2024/25 ni Shilingi 262.2 ambayo ni sawa na asilimia 954.59 ya ongezeko la Bajeti ya Miradi ya Maendeleo”