Na Lucy Lyatuu
MTAFITI kutoka Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) Dk Pendo Ibrahim ameshauri kuwepo muongozo wenye kuwezesha daktari kuchukua hatua za vipimo zaidi pindi anapoona dalili za ugonjwa mwingine Kwa mgonjwa.
Dk Pendo amesema hayo wakati akitoa matokeo ya utafiti wake kuhusu mgonjwa wa saratani ya ngozi ijulikanayo kama Kaposi sacoma ambayo mara nyingi huwapata wagonjwa wenye Virusi vya Ukimwi lakini mgonjwa huyo awali alipopimwa alionekana kutokuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Dk Pendo amesema vifaa vinavyotumika Sasa vinasaidia kutambua mgonjwa mwenye maambukizi ya Ukimwi lakini wapo baadhi wenye maambukizi hayo lakini hawagunduliki Kwa kutumia vifaa hivyo, hivyo kuwepo muongozo Ili daktari akiona dalili zipo achukue hatua zaidi.
Akizungumzia mgonjwa huyo amesema awali alifika katika Hospitali ya Mwananyamala akiwa na dalili za saratani ya ngozi (Kaposi sacoma) ambayo mara nyingi huwapata wagonjwa wa Ukimwi na alipewa rufaa Hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na alipopimwa alionekana na saratani hiyo lakini hakuwa na maambukizi ya Ukimwi.
“Alipofika Muhimbili alipimwa Kwa njia ya kawaida Kwa mujibu wa muongozo ya Tanzania na Bado ha kuonekana na VVU,” amesema Dk Pendo na kuongeza kuwa alipofika wodini Daktari wa wodini alimpima Kwa kutumia kipimo kingine kinachoitwa elaizer na matokeo kuonesha ni kweli ana maambukizi ya VVU.
Amesema daktari alienda mbele zaidi kupima wingi wa Virusi na kukutwa na kopi 700,000 na alipimwa zaidi Kwa kuchukuliwa kinyama Cha ngozi na kukutwa na saratani hiyo na kuanzishiwa dawa.
” Lakini Kwa sababu matibabu ya saratani ni gharama na hakuwa na uwezo alirudi nyumbani bila dawa za saratani na baada ya wiki tatu alirudi akiwa amezidiwa na kulazwa chumba Cha wagonjwa mahututi na baadae alifariki,” amesema.
Amesema pamoja na kwamba hiyo ni tafiti moja walioiona lakini zipo nchi mbalimbali ambazo suala kama Hilo hutokea kutokana na matumizi ya vifaa vya rapid vya kupimia.
Dk Pendo anasema kifo Cha mgonjwa huyo kingeweza kuzuiwa maana alifika vituo vya afya tofauti vitatu na angegundulika mapema angehudumiwa mapema.
Ameshauri kuwa inapotokea wagonjwa wa aina hiyo na daktari kujiridhisha kuwa na tatizo lingine ni vyema kwenda mbele zaidi ya hapo, hivyo iwepo muongozo Kwa madaktari.
Aidha ameshauri kufanyika utafiti zaidi kuona kama Kuna matukio kama hayo mangapi na kwamba watafiti waangalie hayo matukio hayo na kuchukua hatua zaidi.