Na Mwandishi Wetu
BANJUL, Gambia: Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWC25), Profesa Dos Santosi Silayo, amesema bara la Afrika liko kwenye shinikizo kubwa linalotokana na kasi ya mabadiliko ya tabianchi,
Ongezeko la migongano kati ya binadamu na wanyamapori, pamoja na mahitaji mapya ya kijamii na kiuchumi yanayoathiri rasilimali asilia.
Profesa Silayo amesema hayo katika kikao cha 25 cha AFWC kilichofanyika Banjul, akisisitiza kwamba Afrika haiwezi tena kutegemea mbinu za kale katika usimamizi wa misitu na wanyamapori.
“Mabadiliko ya tabianchi yamebadilisha mazingira, tabia za watu zimebadilika, na mienendo ya wanyama imebadilika pia.
“Hatuwezi kuendelea kwa mazoea; tunahitaji ubunifu jumuishi unaotumia sayansi na unaowajibika,” amesema Profesa Silayo.
Ameongeza kuwa sekta inaweza kuimarika ikiwa mataifa yatawekeza katika modeli sahihi za kaboni, teknolojia za kisasa za ufuatiliaji wa misitu, tafiti za mwingiliano wa maji na misitu, mbinu za kupunguza uharibifu wa misitu, na kuimarisha taasisi za jamii ambazo ndizo msingi wa shughuli za uhifadhi.
Katika kikao hicho, Profesa Silayo amekabidhi rasmi uenyekiti kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mazingira ya Gambia, Ebrima Jawara, hatua iliyoweka mwelekeo mpya wa bara katika kukabiliana na changamoto za karne ya sasa. Katika uchaguzi huo, Jawara alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa AFWC25.
Akipokea wadhifa huo, Jawara ameshukuru, akiahidi kuendeleza mageuzi yaliyowekwa na mtangulizi wake na kusisitiza kwamba mustakabali wa uhifadhi wa Afrika unahitaji dira ya pamoja, uongozi unaotegemea ushahidi wa kisayansi, na ushirikiano wa kikanda.
Aidha, viongozi kutoka Rwanda, Chad na Botswana waliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume, uteuzi uliopongezwa na wajumbe kama ishara ya uwakilishi mpana na mshikamano wa kikanda. Wajumbe pia walihakikishia Jawara ushirikiano wa karibu, wakisema:
“Tupo nyuma yako. Tuendelee kulinda rasilimali zetu na kuimarisha sera zetu.”
Katibu wa AFWC, Edward Kilawe, alisema, “Tunategemea ushirikiano wa viongozi wa nchi na wadau wote. Mwenyekiti Jawara na timu yake wana jukumu la kuimarisha usimamizi wa misitu na uhifadhi wa wanyamapori barani Afrika kwa njia endelevu na ya kisayansi.”
Wajumbe pia walimpongeza Profesa Silayo kwa uongozi wake katika kipindi kilichokabiliwa na changamoto za tabianchi, ongezeko la shinikizo la ardhi, na mahitaji mapya ya kiuchumi.
AFWC25 ni kikao cha kikanda cha wakuu wa sekta ya misitu na wanyamapori barani Afrika, kilichokutana kwa mwaka wa 25 mfululizo kujadili changamoto, kushirikiana mbinu za kisayansi, na kuboresha sera za uhifadhi. Kikao cha mwaka huu, kilichoanza Desemba mosi hadi tano, 2025,.
Kimehusisha wajumbe kutoka nchi zote za Afrika, wakijadili mwelekeo wa usimamizi wa misitu, migongano kati ya binadamu na wanyamapori, na mbinu za kuendeleza mageuzi endelevu ya sekta hiyo.

