Na Lucy Ngowi
DODOMA: BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limefanya uchaguzi wa Spika wake mpya, ambapo Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, amechaguliwa kwa ushindi wa kishindo kuwa Spika wa Bunge la 13.
Zungu amepata kura 378 kati ya kura zote zilizopigwa na wabunge, na hivyo kumpa nafasi ya kuliongoza chombo hicho muhimu cha kutunga sheria.
Uchaguzi huo umefanyika leo Novemba 11, 2025, jijini Dodoma, katika kikao cha kwanza cha Bunge jipya baada ya uchaguzi mkuu.
Kwa ushindi huo, Zungu anachukua jukumu zito la kusimamia shughuli zote za Bunge, kuhakikisha uwajibikaji wa serikali, na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya wabunge kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania.
Katika kinyang’anyiro hicho, wagombea wengine walikuwa Veronica Tyeah (NRA) kura 0, Anitha Mgaya (NLD) kura 0, Chrisant Nyakitita (DP) kura 0, Ndonge Ndonge (AAFP) kura moja na Amin Yango (ADC) kura moja.
Ushindi wa Zungu unaashiria kuungwa mkono kwa wingi na wabunge wenzake, huku wengi wakieleza matumaini kuwa ataendeleza misingi ya umoja, nidhamu, na uwazi ndani ya Bunge hilo jipya.

