Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Hospitali ya Ocean Road, Dkt. Faraja Kiwanga, amesema mwezi huu wa Oktoba ni wa kuhamasisha uelewa kuhusu ugonjwa wa saratani ya matiti, ambao unaweza kuzuilika na kutibika iwapo utagunduliwa mapema.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, katika mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kuongeza uelewa kwa wanahabari kuhusu ugonjwa huo, Dkt. Kiwanga amesema saratani hutokea pale chembe hai za mwili zinapobadilika tabia zake za kawaida na kuanza kukua kwa kasi isiyo ya kawaida.
Amesema kwa sasa kuna zaidi ya aina 100 za saratani, ambazo huathiri watu wa rika zote wakiwemo watoto na watu wazima.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, kila mwaka watu zaidi ya milioni 11 duniani hugundulika na saratani, huku milioni tisa wakipoteza maisha, na zaidi ya milioni 43 wakiishi na ugonjwa huo.

Dkt. Kiwanga amesema nchini Tanzania, kwa kila watu 100,000, takriban wagonjwa 76 hugundulika na saratani, huku wagonjwa wapya 42,000 wakirekodiwa kila mwaka na takribani 28,000 wakifariki dunia kutokana na maradhi hayo.
Amesema changamoto kubwa ni wagonjwa wengi kufika hospitalini kwa kuchelewa, ambapo asilimia 75 ya wagonjwa hufika wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo.
Kwa upande wa wanaume, saratani zinazoongoza ni za tezi dume, utumbo mkubwa na mdogo, huku kwa wanawake saratani ya mlango wa kizazi ikiongoza kwa asilimia 47, ikifuatiwa na saratani ya matiti (asilimia 16) na saratani ya koo.
Ametaja visababishi vinavyoweza kuzuilika kuwa ni pamoja na mtindo wa maisha usiofaa, ulaji wa vyakula vilivyokaa muda mrefu na kuota ukungu kama karanga na korosho, unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi, na athari za kemikali za viwandani.
Dkt. Kiwanga amesema kwa wanawake, vichocheo vya saratani ya matiti ni pamoja na kuanza hedhi mapema, kuchelewa kukoma hedhi, kutokuzaa au kuzaa kwa umri mkubwa, kutonyonyesha, unene uliopitiliza, na matumizi ya pombe kupita kiasi.
Dalili kuu za ugonjwa huo ni uvimbe kwenye titi au kwapa, na amewataka wananchi kufika hospitalini mapema pindi wanapogundua mabadiliko yoyote.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji TAMWA, Dkt. Rose Reuben, Meneja wa Mipango Mkakati Sylivia Daulinge, amesema mwezi huu Oktoba ni muhimu kwa ajili ya kuelimisha jamii na kuwaenzi wote waliopitia changamoto ya saratani.
Amesema waandishi wa habari wana wajibu mkubwa wa kutumia kalamu zao kueneza elimu na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ugonjwa huo, huku akishukuru Hospitali ya Ocean Road kwa ushirikiano na utayari wao katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa saratani.

