Na Mwandishi Wetu
BARIADI VIJIJINI: MGOMBEA urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amewataka wananchi wa Bariadi kujitokeza kwa wingi kupiga ‘kura ya ukombozi wa hasira’ ifikapo Oktoba 29, mwaka huu.
Akihutubia mkutano wa kampeni za lala salama, Mwalim amesema kura hiyo ndiyo suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwemo matatizo ya huduma za afya, bei ya pamba na hali ngumu ya wafugaji.

“Acheni kukumbatia CCM. Nendeni mkapige kura ya ukombozi wa hasira kwa CHAUMMA ili msije kujutia maamuzi yenu,” amesema Mwalim.
Ameongeza kuwa wananchi wasipofanya maamuzi sahihi mwaka huu, atarejea mwakani kuuliza kama wamekomboa maisha yao au wameendelea kuteseka kwa kukibakiza madarakani chama kilichosababisha umaskini wao.
Mwalim pia amelaani vitendo vya uonevu vinavyowakumba wananchi katika maeneo yaliyopakana na hifadhi, pamoja na kukamatwa holela kwa vijana, akisisitiza kuwa mabadiliko hayo yanawezekana tu kupitia kura ya Oktoba 29, mwaka huu 2025.

