Na Lucy Ngowi
KATIKA siku za karibuni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kilisaini mkataba wa ujenzi wa Mradi wa Elimu ya Juu Tanzania kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET).
Utiaji saini huo ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali za kuboresha elimu ya juu na kuimarisha mazingira ya kujifunza na kufundishia nchini.
Kwa kuwa mradi huo wa kuboresha elimu ya juu nchini Tanzania unasaidia ukuaji wa uchumi kwa kuimarisha vyuo vikuu, utafiti na ujuzi wa wanafunzi katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda anasema chuo hicho kimesaini mkataba wa ujenzi wa maabara tatu na Mkandarasi Arm Strong Int. Ltd, ambao utakuwa ni wa miezi nane.
anasema mkataba huo uliosainiwa wa ujenzi wa maabara hizo upo chini ya chuo hicho kupitia Mradi wa HEET.
Anasema mradi wa HEET hauwezi kuwa wa maana kama vitafanyika vitu ambavyo havitaleta mabadiliko katika jamii.
“Uwepo wa mradi huu ni sehemu ya maeneo saba ya utekelezaji wa HEET. Tunalenga kujenga maabara za kisayansi, tunatambua nchi haiwezi kuendelea au kubadilika bila kuweka msisitizo kwenye sayansi,” anasema.
Anasema mkandarasa waliyeingia naye mkataba atajenga maabara tatu katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Kigoma. Maabara nyingine zilizobakia zitajengwa na wakandarasi tofauti tofauti.
Naibu Makamu Mkuu wa OUT upande wa Taaluma, Tafiti na Huduma za ushauri. Profesa Alex Makulilo anasema mradi huo unaotekelezwa na chuo hicho kwa thamani ya dola milioni tisa.
Anasema fedha hizo zimegawanyika katika vipengele mbalimbali , kwani asilimia 75 ya mradi mzima zinaenda kwenye ujenzi, maabara saba katika Kanda saba.
Anasema mradi huo ni sehemu ya mpango wa Serikali unaotekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ili kuimarisha elimu ya juu kupitia uwekezaji katika miundombinu, teknolojia na rasilimali watu.
Anasema chuo kikuu huria ni miongoni mwa taasisi 22 za elimu ya juu chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zinazofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Katika kutekeleza mradi huu OUT kimetengewa Dola za Kimarekani milioni tisa na unalenga kupanua na kuboresha mazingira ya kujifunzia, ikijumuisha
kuimarisha miundombinu ya kidijitali, rasilimali za mtandaoni, kujenga uwezo wa kitaaluma, na kuwanoa wafanyakazi katika mbinu za kisasa za ufundishaji, utafiti na ubunifu.
“Mradi huu pia una lengo la kupunguza pengo la kijinsia katika masomo ya sayansi na teknolojia kwa kuwawezesha wanawake kushiriki kwa wingi katika programu za STEM.
“Tunatambua kuwa maendeleo ya taifa lolote yanategemea rasilimali watu wenye ujuzi wa hali ya juu, hususan katika nyanja za sayansi na teknolojia, hivyo uwekezaji huu ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu,” anasema.
Anasema OUT kitajenga majengo saba katika mikoa ya Arusha, Mwanza,Kigoma, Morogoro, Pwani, Mtwara na Njombe kwa matumizi mbalimbali, kila jengo litakuwa na maabara sita za sayansi katika kila moja ya vituo saba vya kikanda .
Anasema kila kituo kitahudumia angalau mikoa mitatu., na kwamba maabara hizo zitatumika kama sayansi katika maeneo ya kipaumbele ya mradi.
Anasema pia majengo hayo yatakuwa na kituo cha TEHAMA, sehemu ya mafunzo ya vitendo kwa ukarimu na utalii, pamoja na maghala ya kuhifadhia vifaa na ofisi kwa wafanyakazi wa maabara.
Anasema chuo kinaishukuru serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya elimu kama nyenzo kuu ya maendeleo. Kupitia mradi huo wa HEET wanaamini utasaidia kuongeza fursa kwa wanafunzi wengi zaidi kupata elimu yenye ubora wa kimataifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Arm Strong Int. Ltd, Pastory Masota anasema wakandarasi ni watekelezaji wa mradi ukiooitia michakato mingi, kupitiwa na watu wengi.
Anasema wao wataweka yote waliyokubaliana katika hali halisi.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Joseph Kuzilwa anasema kuna uhusiano mkubwa kati ya uwekezaji wa elimu na ukuaji wa uchumi.