Akabidhiwa Cheti Ishara ya Kutambua Mchango Wake Kwa Jamii, Utafiti Alioufanya Wenye Matokeo Chanya
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WATAFITI na Wabunifu hapa nchini wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto katika jamii.
Kutokana na kufanyika kwa tafiti hizo, mara nyingi serikali imekuwa ikisisitiza kuwa zitumike kutatua changamoto mbalimbali badala ya kuzifungia kabatini.
Hivi karibuni Naibu Waziri Mkuu Dkt. Dotto Biteko alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la tisa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, lililoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia lililofanyika Mkoani Dar es Salaam.
Katika kongamano hilo, Biteko aliagiza kuwatumia wanasayansi wa ndani ya nchi badala ya kuwavunja moyo katika tafiti zao wanazozifanya ambazo zinazotatua changamoto zilizopo katika jamii.
Maelezo ya Dkt Biteko ni kwamba, umefika wakati wa serikali, taasisi na mashirika kutambua, kuthamini na kutumia tafiti za wanasayansi wa ndani ya nchi zinazotatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.
Katika hilo anasema wanasayansi nchini wanafanya kazi nzuri na kubwa ya kutafuta suluhu ya matatizo mbalimbali katika jamii lakini kazi zao zinatambuliwa zaidi nje ya nchi kuliko nchini jambo ambalo linaweza kuwavunja moyo.
Pia katika kongamano hilo Biteko aliweza kutambua mchango wa wanasayansi ambao tafiti zao ni miongoni mwa tafiti bora zilizoweza kutatua changamoto za kijamii kwa kuwapa tuzo.
Mmoja wa watafiti waliokabidhiwa tuzo ya wanasayansi bora katika kongamano hilo, ni Dkt. Aviti Mmochi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye anashughulika na Uchumi wa buluu.
Dkt. Mmochi anasema tuzo aliyopewa imetokana na utafiti katika ufugaji wa samaki, pamoja na viumbe mbalimbali vya bahari, kuwa ni samaki aina ya Mwatiko, Mkizi, Chaza pia majongoo bahari na mwani.
‘’Hapo nyuma viumbe hivi vya baharini vilikuwa havifugiki lakini tumeweza kuvifuga. Mfano ufugaji wa samaki aina ya mwatiko ambao tulianza nao miaka ya 2000 hadi 2005, lakini tuliwaendeleza toka 2005 mpaka sasa tunaendelea nao.
“Samaki hawa wametoka kwenye tani sifuri lakini kupitia takwimu za Shirika la Chakula Duniani walikuwa wamefika tani 240 na wanaendelea,’’ anasema.
Anasema pia wameweza kufuga samaki aina ya Perege kwenye maji baridi na maji ya chumvi.
“Ni kweli samaki wote wanaopatikana mito ya Pangani, Rufiji mpaka Ruvuma kwa kuwa wameingiliana na bahari wame adapt na wanafugika kwenye bahari yetu, na pengine kinachofurahisha zaidi, tuliweza kuzalisha samaki chotara kwa kutumia Samaki dume wa Rufiji na samaki jike wa Ziwa Victoria yaani sato.
‘’Yule Sato wa kike akizaa na Rufiji au Wami wa kiume anazaa madume matupu bila kutumia homoni yoyote.
‘’ Na yale madume yana faida kubwa kwa sababu katika samaki anayeteseka baharini ni sato, lakini vile vifaranga vyake huwa vina uwezo wa kuweza kuishi kwenye maji yoyote,” anasema. Na pia samaki dume wanakuwa wakubwa zaidi na kulingana ukubwa mambo mawili yanayovutia wanunuzi.
Dkt. Mmochi anasema kinachofurahisha ni kwamba chotara hawa wanakuwa haraka zaidi kwenye yale maji ya mchanganyiko kuliko maji ya bahari au maji ya kawaida.
Anasema kwa hiyo samaki hao wanaweza wakalimwa kwenye maji ya chumvi na ya kawaida na kuongeza biashara.
Anaongeza kuwa samaki wengi wanaoweza kulimika hawajulikani na kutolea mfano wa aina ya mwatiko.
‘’Lakini Sato na hao wengine katika kundi la perege wanajulikana duniani kote,” anasema.
Anazungumzia kipengele kingine kuwa ni wamefanikiwa kufuga majongoo bahari na kwamba mazoezi ya ufugaji wa majongoo baharini hapa Tanzania yalianza kufanyika miaka ya 2000 mwishoni baada ya kuonekana yameisha baharini na uokotaji wake umefungwa.
“Kwa hiyo tukafikiri ni wakati maalum wa kuanza kuwafuga na hawa majongoo. Majongoo wanafugwa vizuri wala hawahitaji chakula, hawahitaji chochote wao wanakula matope na kwa maana hiyo wana uwezo wa kuondoa hewa ukaa kwenye bahari ambacho ni kitu muhimu sana na kinasisitizwa katika kupunguza mabadiliko ya tabia nchi, ‘’anasema.
Jambo lingine anasema wameanza kilimo cha mseto cha majongoo bahari na mwani, lakini pia majongoo hayo na samaki aina ya mwatiko.
“Tumegundua kupata zao zaidi ya moja kwenye eneo moja ni faida kubwa zaidi kiuchumi. Majongoo yanauzwa kwa bei kubwa kuliko mazao mengine yoyote ambayo tumewahi kuyapata kwenye bahari yetu kwa maana ya kwamba, katika soko la kawaida kilo ya majongoo inaweza ikafika dola 38, lakini wanaweza kwenda mpaka dola 80.
‘’Ila huko kwao wakifika kilo moja ya jongoo tunayemlima kwa sasa anafika dola 1800. Ni moja ya chakula chenye thamani kubwa kwa wachina ambacho kiko katika vyakula vyao vitano ambavyo vinahusisha konokono,Makome wanaofugwa Afrika ya Kusini.
“Kwa kweli tumefanya vitu vingi kwenye bahari na hiyo ndiyo imefanya kupewa tuzo ya mwanasanyansi ambaye matokeo ya tafiti zake yameweza kumpa tuzo ya ubunifu ulioweza kufika kwa wananchi na kuwatajirisha,” anasema.
Pia ameongeza kuwa eneo lingine walilolitengeneza ni la mwani kwamba wakulima wao badala ya kuuza mwani ghafi ambao bei ni 1000 kwa kilo, na hiyo kilo inatoka kwenye kilo 100, kwa maana kwamba ni asilimia 10 ya mwani mbichi kwa hiyo kiasi kikubwa sana kinapungua.
“Maana yake unauza kwa bei ndogo. Sasa wale wajasiriamali wamejifunza kusaga ule mwani na kuuza unga, vipodozi zikiwemo sabuni na pia kuwekwa kwenye vyakula na viungo mbali mbali vya vyakula, juisi, jamu, visheti nk” anasema.
Anaeleza manufaa ya mwani kuwa ni pamoja na kuondoa magonjwa mbalimbali, una virutubisho aina ya chuma ambavyo vinahitajika kwenye mwili kwa ajili ya virutubisho. Watu wengi waliotumia vyakula au vipodozi vinavyotengezwa na mwani wametoa shuhuda mbali mbali za kupona magonjwa ya ngozi, na viungo .
akiwatambulisha wanasayansi hao waliopewa tuzo, Katibu Mkuu Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Carolyne Nombo anasema kwa mara ya kwanza wizara hiyo kupitia Costech imetoa tuzo hizo katika kongamano hilo la STICE-2024.
Kwamba Dkt. Mmochi ametambuliwa katika eneo la uvuvi kwa kuhusika na tafiti za ufugaji wa viumbe maji wakiwemo samaki wa maji chumvi, chaza na majongoo bahari.
Pia ameshiriki miradi mikubwa na kwa kupitia juhudi zake amekuwa na mchango kwenye ajenda ya uchumi wa buluu.