Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewasilisha bunifu mpya ya dawa za asili kwa ajili ya matibabu ya malaria, vidonda vya tumbo, na ugonjwa wa kisukari.
Utafiti wa dawa hizo umefanywa kuunga mkono juhudi za kitaifa za kutatua changamoto za kiafya kwa njia endelevu na salama.
Akizungumza katika banda la UDOM kwenye maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba, Mtafiti wa Mradi huo ambaye ni mhadhiri chuoni hapo, Dismas Tullo amesema utafiti huo unalenga kutumia rasilimali za asili zilizopo nchini hasa mimea tiba kuandaa dawa mbadala salama kwa magonjwa yanayoathiri watanzania kwa kiwango kikubwa.
“Tumegundua kuwa mimea mingi ambayo inatupwa au haithaminiwi ina uwezo mkubwa wa kiafya. Ndiyo maana tumeamua kufanya tafiti na kuzalisha dawa ambazo zitatatua changamoto halisi katika jamii,” amesema.
Akielezea dawa ya kisukari ya Gymerine amesema inalenga kupunguza kiwango cha sukari mwilini kwa wagonjwa wa kisukari.
Amesema dawa hiyo imefanyiwa majaribio ya awali katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), ambapo baadhi ya wagonjwa waliotumia dawa hiyo wameonyesha maendeleo chanya ya kiafya.
Kwa upande wa matibabu ya vidonda vya tumbo, UDOM imebuni dawa iitwayo Ulcerexia, ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua ya majaribio ya kitabibu.
Wagonjwa wa awali waliotumia dawa hiyo walionyesha hali nzuri ya kupona, huku tafiti zaidi zikiendelea kuthibitisha usalama na ufanisi wake kwa matumizi ya binadamu.
Amesema katika mapambano dhidi ya ugonjwa sugu wa malaria, chuo hicho kimebuni dawa mpya iitwayo Malaherb, ambayo imeundwa kwa kutumia mimea ya asili yenye uwezo wa kupambana na vimelea vya malaria.
Tofauti na dawa mseto inayotumika kwa sasa na kuhitaji vidonge vingi kwa dozi moja, Malaherb imetengenezwa kwa kuzingatia urahisi wa matumizi kwa mgonjwa.
“Wagonjwa wengi wa malaria wanashindwa kumaliza dozi ya dawa mseto kwa sababu ya idadi kubwa ya vidonge.
“Hali hiyo hupelekea ugonjwa kurudi au kusababisha madhara mengine kama matatizo ya figo. Malaherb ni dozi rafiki, rahisi kutumia, na isiyo na madhara ya sumu,” alisema Tullo.
Mbali na dawa hizo, Tullo alibainisha kuwa chuo hicho pia kimebuni bidhaa za lishe maalum kwa wagonjwa wa kisukari, wagonjwa wa ini, watoto wenye utapiamlo pamoja na watu wanaoishi na VVU. Bidhaa hizo zinalenga kuboresha kinga ya mwili na kusaidia katika kuimarisha afya kwa kundi hilo maalum la watu.
“Tunachokifanya ni kuleta sayansi kwenye tiba za asili kwa kuhakikisha kuwa bidhaa tunazozalisha ni salama, zinafanyiwa majaribio na zina viwango vya kitaalamu vinavyokubalika,” amesema.