Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM:. MfFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), utaongeza wigo wa hifadhi ya jamii na kuwafikia wananchi waliojiajiri waweze kujiunga na kuchangia ili wanufaike na mafao mbalimbali yanayotolewa.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, leo Machi 14 , 2025, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, Mshomba amesema mfuko huo unaendelea
kutimiza azma ya serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema suala la wananchi kujiunga na kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii ni ajenda ya dunia na ya nchi na kuwa lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama, ambapo serikali imelipa umuhimu wa pekee.
“Ninakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo umelishikia bango jambo hili, umeshirikiana na sisi tangu tuanze kampeni yetu ya “NSSF Staa wa Mchezo”,

“Kuhakikisha waliojisajili wanakuwa sehemu ya hifadhi ya jamii kama ambavyo nchi zilizoendelea zimewasajili wananchi waliojiajiri,” amesema,
Amesema kwa mujibu wa malengo 17 ya dunia, kila lengo linazungumzia masuala ya hifadhi ya jamii kwa sababu ili uweze kuondoa umasikini ni hatua ya kwanza wananchi wa taifa husika wawe ni wanufaika wa hifadhi ya jamii,

Kwa sababu kupitia hifadhi ya jamii mwanachama au mwananchi anakuwa na uhakika wa maisha na kipato.
“Ndio maana tunasema “NSSF Staa wa Mchezo” kwa maana ukiwa mwanachama wa NSSF wewe utang’aa, utakuwa Staa katika maisha yako yote, wakati ukiwa na nguvu za kufanya kazi na hata baada ya kumaliza kufanya kazi,
“NSSF inakuwa Staa wa kukupa pensheni ya uzee, hivyo nawaomba wananchi waendelee kujiunga na kuchangia ili wawe Mastaa wa Mchezo wa sasa na baadaye,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri Ridhiwani amesema tayari amezindua kampeni ya “NSSF Staa wa Mchezo” yenye lengo la kuwanufaisha wananchi waliojiajiri katika sekta mbalimbali,
Zikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji, uchimbaji wa madini, waendesha bodaboda, mama/baba lishe na wajasirimali wengine wote ili waweze kunufaika na mafao na huduma nyingine zinazotolewa na Mfuko.

Amesema uamuzi wa NSSF kuzindua kampeni hiyo ni hatua kubwa iliyofikiwa yenye lengo la kuongeza wigo katika hifadhi ya jamii na kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na mafao ya muda mrefu na muda mfupi yakiwemo ya matibabu.