Na Waandishi Wetu
WAZIRI wa Mambo ya Nje nchini China, Wang Yi amesisitiza kanuni za kushauriana kwa pamoja, kujenga kwa pamoja na kunufaika kwa pamoja katika ushirikiano baina ya nchi.
Waziri huyo anasisitiza kanuni hizo katika Mkutano wa Waandishi wa Habari wa tatu wa Bunge la 14 la Umma la China.
Katika mkutano huyo anahimiza uwepo mshikamano baina ya China na nchi nyingine duniani kwa maendeleo ya pamoja, hususani watu wa Dunia ya Kusini.
Vile vile anaelezea mipango 10 ya ushirikiano iliyotolewa katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika Beijing, China, Septemba nne hadi sita, mwaka jana 2024.
Anasema mipango hiyo itaendelea kutekelezwa hatua kwa hatua ili kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Afrika.
Kauli yake imeonyesha falsafa ya Kichina Tianxia Wei Gong – ‘Dunia ni ya Walimwengu Wote’ na maendeleo yake katika enzi ya kisasa.
Falsafa hiyo imedhihirisha dhamira thabiti ya China ya kukuza maendeleo ya dunia yenye amani.
Fikra ya Tianxia Wei Gong ilitokana na kitabu cha kale cha Kichina.
Katika vipindi viwili vya 770 K.K.-221 K.K. wanazuoni wa kundi la Confucius walipendekeza fikra za “Datong” na “Tianxia Wei Gong”, yaani wanajamii wote wangeishi kwa furaha na amani wakisaidiana maishani, huku viongozi wa taifa wakiboresha maisha ya watu na kutawala nchi kwa haki na usawa.
Falsafa hiyo baadaye ilichukuliwa kama kigezo cha jamii bora, na hatimaye ikawa falsafa inayoongoza diplomasia ya kisasa ya China.
Katika zama za leo, fikra hii imepewa maana mpya. Wazo la kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja linatokana na fikra hiyo, likiakisi tafakari ya China kuhusu usimamizi wa kimataifa.
Dunia ya leo inakabiliana na matatizo mbalimbali, yakiwemo msimamo wa upande mmoja, sera za kujilinda kibiashara na nyinginezo.
Ili kuzitatua changamoto hizo nchi zinazoendelea zinazidi kushirikiana na kulinda utaratibu wa pande nyingi na usawa wa kimataifa.
Hii imekuwa mkondo wa dunia, pia inaendana na falsafa ya Tianxia Wei Gong.
Ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Afrika ni mfano mzuri wa falsafa hiyo.
Tangu kuasisiwa kwa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), uhusiano kati ya China na Afrika umepata maendeleo makubwa.
Maendeleo hayo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu, ushirikiano wa afya, mafunzo ya kuwatayarisha weledi na ubunifu wa kisayansi.
Kwamba matunda ya ushirikiano kati ya China na Afrika yamenufaisha watu wa pande mbili, China ikiwa mbia mkubwa zaidi wa biashara wa Afrika kwa miaka 16 mfululizo.
Zaidi ya hayo, China na Afrika zimeanzisha majukwaa mbalimbali ya kuhimiza ushirikiano, yakihimiza mfumo katika maeneo mbalimbali.
Na kwa kupitia mazungumzo yenye usawa na ubadilishanaji wa mawazo, pande zote zinaweza kupata suluhisho la kutatua changamoto za kimataifa kama vile mabadiliko ya tabianchi, changamoto ya kiteknolojia, masuala ya usalama, tofauti za kitamaduni na nyinginezo.
Zaidi ya hayo, ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Afrika umeongezea dhana ya Dunia ya Kusini undani mpya.
Zamani, machoni mwa watu wengi, dhana hiyo ilihusiana na kiwango cha chini cha maendeleo.
Hali hiyo ilisababishwa na ukosefu wa sauti na uwakilishi wa nchi za Dunia ya Kusini katika mfumo wa usimamizi wa dunia.
Lakini sasa, nchi za Dunia ya Kusini zimeanza kutoa sauti zao: ziko tayari kushiriki katika usimamizi wa dunia, zikitoa mawazo na mchango muhimu kwa maendeleo ya kimataifa katika sekta ya siasa, uchumi, viwanda, elimu, utamaduni na nyinginezo.
Aidha, urithi wao wa kitamaduni, uzoefu wao wa kupata maendeleo, na mbinu zao bunifu za utawala zimetoa suluhisho mpya kwa changamoto za kimataifa.
Hivi sasa nchi za Kusini zinashiriki katika utungaji wa kanuni za kimataifa na kuboresha mfumo wa ujuzi wa kimataifa, ili kuhakikisha mfumo wa usimamizi wa kimataifa uwe na haki na usawa.
Kama Confucius alivyosema, ‘Penye wanafunzi, hapakosi walimu’ Katika mchakato huo watu wa China wameshuhudia hekima na nguvu za watu wa Afrika, wanaamini kuwa Afrika bila shaka itatoa mchango mkubwa zaidi katika siku zijazo.
Kwa pamoja China na Afrika zinaleta maendeleo, amani na utulivu katika dunia jambo ambalo ni muhimu kwenye historia.
Mwaka huu 2025 mipango 10 ya ushirikiano iliyotolewa kwenye Mkutano wa FOCAC itaendelea kutekelezwa.
Ni imani kuwa Wachina na Waafrika watafuata falsafa ya Tianxia Wei Gong, kwa ajili ya maendeleo duniani yenye haki, usawa na amani.
Waandishi Li Hongfeng na Wei Yuanyuan
Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing, China