Na Danson Kaijage
DODOMA: MWAKA wa fedha 2024/25 Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania umepata ongezeko la Sh. Bilioni tatu tofauti na mwaka wa fedha 2023/24 ambapo ulikuwa na bajeti ya Sh. Bilioni1.6.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania Nyakaho Mahemba, alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya utekelezaji na Maendeleo ya mfuko huo kwa muda wa miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akielezea mafanikio hayo amesema, awali bajeti ya mfuko huo ilikuwa chini ya kiwango cha uendeshaji na uboreshaji wa mfuko,suala lililokuwa likipunguza ufanisi wa utendaji.
Pia amesema tangu kupatikana kwa uhuru mfuko huo haujawahi kuwa na bajeti kubwa kama ilivyo sasa.
Kwa maelezo yake, sekta ya utamaduni ilikuwa ikipata ruzuku ya Sh.Milioni 500 ambayo ilikuwa haiwezi kukidhi malengo ya sekta hiyo na baadaye katika mwaka wa fedha 2023/24 iliidhinishwa bajeti ya Sh. Bilioni 1.6.

Na mwaka wa fedha 2024/25 ikaidhinishwa Sh.Bilioni tatu jambo ambalo halijawahi kutokea katika sekta hiyo.
Amesema kiasi kilichoongezeka ni Sh. Bilioni 1.4 ambacho ni sawa na ongezeko la asilimia 87.5 huku
Serikali ikiongeza chanzo kipya na endelevu cha mapato ya Mfuko kinachotozwa katika vibebeo tupu vya Kazi za Sanaa (Tozo ya Hakimiliki).
Ameeleza kuwa , kupitia chanzo hicho, Mfuko hupata gawio la asilimia 10 ya mapato yote yanayokusanywa na chanzo hiki kimeanza kutekelezwa Mwezi Septemba, 2023.
Katika hatua nyingine amesema kuwa mfuko umefanikiwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
mikopo yenye thamani ya Sh. Bilioni 5.2 kwa miradi 359 ya Sanaa iliyozalisha jumla ya ajira 497,213.
Akielezea mchanganuo wa miradi aliyataja maeneo ya miradi iliyowezeshwa ni muziki (miradi 78), filamu (miradi 90), maonesho (miradi 65), Ufundi (miradi 103) na Lugha na Fasihi (23).
Pia ameitaja Mikoa iliyofikiwa ni 18 ambayo ni Dar- Es Salaam, Arusha, Morogoro, Pwani, Geita, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Kagera, Mara, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Simiyu, Kigoma na Katavi.