Na Mwandishi Wetu
MUSOMA – MARA: MGOMBEA urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amesema hakuna mamlaka yoyote, iwe ya ndani au ya kimataifa, inayoweza kuzuia mchakato wa uchaguzi nchini, akisisitiza kuwa huo ni msingi wa haki ya kikatiba kwa wananchi.

Amesema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa wazi mjini Musoma, Mkoa wa Mara.
Mwalim amesema taasisi ya upinzani imejengwa kwa juhudi na gharama kubwa kwa miaka mingi, na hivyo haiwezi kuruhusu kuvurugwa kwa mchakato wa kidemokrasia kwa sababu zisizo na msingi.
“Uchaguzi ni njia halali ya kuleta mabadiliko. Hakuna sheria inayoruhusu mtu binafsi au taasisi yoyote kuuzuia. Hata taasisi za kimataifa hazina mamlaka hayo,” amesema.
Ameonya vikali dhidi ya kile alichokitaja kama njama za makusudi za kuhujumu demokrasia kwa kisingizio cha migogoro au misimamo ya kisiasa.
“Kususa uchaguzi si suluhisho. Ni kosa la kiufundi katika siasa za kimageuzi,” amesema.
Kauli ya Mwalim imekuja wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikizidi kushika kasi, huku vyama vya siasa vikiendelea kujipanga kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani.