Na Mwandishi Wetu
PWANI: WATOTO wenye mahitaji maalum wamepatiwa aina 25 ya vifaa ili viweze kuwasaidia.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amekabidhi vifaa hivyo kwa watoto hao wenye mahitaji maalum.

Pia Ridhiwani ameishukuru serikali
Kwa kuendelea kutoa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Katika hatua nyingine, Ridhiwani ameishukuru Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze kwa usimamizi mzuri wa fedha na kutoa elimu kwa wazazi ili kuona umuhimu wa kuwapeleka shule watoto hao.
Akitoa msaada huo ameahidi kuwa serikali itaendelea kupeleka fedha ili kukamilisha ujenzi wa mabweni.

Vile vile amesema kupitia Mfuko wa Jimbo, wametoa madawati 500, wataendelea kuhakikisha wanasaidia ili kutatua changamoto zilizopo na kuweka mazingira mazuri kwa watoto ili waweze kusoma kama wengine.
Amewapongeza walimu wanaofundisha watoto hao .

Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Elimu msingi na Awali Miriam Kihiyo, Ofisa Elimu maalumu wa Halmashauri ya Chalinze Divisheni ya Awali na msingi Elikana Lukuba amesema bado kuna changamoto mbalimbali, na kuishukuru halmashauri hiyo inavyojitahidi kutenga fedha,
Kwenye bajeti kupitia mapato ya ndani na kupunguza changamoto hizo kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa Elimu.
Ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kutoa mwongozo kwa walimu waliosomea elimu maalumu ambao wanafundisha shule zisizo na wanafunzi wenye mahitaji maalumu kuwaajiri kwenye Shule zenye uhitaji huo.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya shule ya Msingi Chalinze kitengo cha elimu maalumu ameishukuru Serikali kwa kuwapatia vifaa hivyo na kwani vitakuwa msaada mkubwa kwa watoto hao.