Na Lucy Ngowi
TANGA:WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amesema marehemu Ernest Kimaya, atakumbukwa kutokana na jitihada mbalimbali alizofanya za mabadiliko ya sera zinazosimamia ustawi wa wenye mahitaji maalum.
Marehemu Kimaya alikuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) na Mjumbe wa Baraza la Taifa la Ushauri Kwa Watu Wenye Ulemavu.
Ridhiwani amesema hayo wakati wa mazishi ya Kimaya yaliyofanyika katika Kijiji cha Mnyuzi Wilaya ya Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.

Amesema marehemu huyo pia kati harakati mbalimbali za kutetea watu wenye mahitaji maalum.
“Namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai wa Kimaya ambaye alianza harakati za kutetea watu wenye mahitaji maalum toka akiwa na miaka 19 miaka ya 1990.
“Kimaya ambaye amewahi kushiriki katika harakati mbalimbali atakumbukwa kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa Mbunge wa Bunge maalum,” amesema Ridhiwani.
Katika mazishi hayo Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh. Milioni tatu za rambirambi kwa familia zilizopokelewa na binti yake Elizabeth.

Kimaya alifariki Disemba 30, 2024 Jijini Dar es Salaam katika hospitali ya Ocean Road ambapo alikuwa akipatiwa matibabu.