Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MASHINE mpya ya kupandia ya ‘ Rafiki Planter’ iliyobuniwa na watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Ukirigulu mkoani Mwanza, inaleta mapinduzi ya kweli mashambani hivyo kuwawezesha wakulima kutumia muda mchache wawapo shambani.
Akiwa kwenye maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba, Mtafiti kutoka TARI Ukiliguru, Dauson Malela ameielezea mashine hiyo kuwa ni ndogo, nyepesi na rahisi kutumia, imeundwa mahsusi kuwasaidia wakulima kupanda mazao kwa haraka, ufanisi, na kwa gharama nafuu.
Amesema mashine hiyo imeundwa kwa mfumo unaofanana na boda boda au bajaji hivyo Rafiki Planter ni chachu ya kuwavutia vijana kuingia kwenye kilimo chenye tija.
Amesema mashine hiyo inayotumia petroli lita moja kwa ekari moja, ina uwezo wa kupanda mazao kama mahindi, pamba na alizeti kwa kutumia saa moja tu kumaliza ekari moja.
“Tofauti na matumizi ya jembe la mkono yanayohitaji watu nane hadi 12 kutumia saa sita hadi nane pamoja na gharama ya ujira wa kati ya Sh. 40,000 hadi 60,000 kwa ekari, Rafiki Planter huokoa muda na fedha kwa kiwango kikubwa.
“Hii si tu mashine ya kupanda ni nyenzo ya kumkomboa mkulima na kumfanya awe mzalishaji wa kisasa. Ni mkombozi wa kilimo, hasa kwa vijana,” amesema.
Nyenzo Rahisi Ndio Kichocheo cha Vijana Kuingia Kwenye Kilimo
Amesema Serikali kupitia mpango wa ‘Building a Better Tomorrow’ (BBT) imekuwa ikihimiza vijana kushiriki katika kilimo cha kisasa lakini changamoto imekuwa zana duni lakini mashine hiyo imekuwa suluhisho.
Amesema Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Ukirigulu, Dkt. Sabas Saidia ameshiriki kikamilifu katika utafiti na utengenezaji wa mashine hiyo pamoja na wataalamu wengine akiwemo Mtaalamu wa mbegu kituoni hapo, Robert Cheleo.
Amesema baada ya kufanyiwa majaribio katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Simiyu na Geita, mashine hiyo sasa ipo tayari kuingia sokoni.
“Maoni ya wakulima yamezingatiwa na maboresho kufanyika na sasa zaidi ya wakulima 50 wameonyesha nia ya kuinunua katika maonesho ya 49 ya biashara yanayoendelea.
“Kwa sasa, TARI imeingia makubaliano na Taasisi ya Usambazaji wa Zana Rahisi Vijijini (CAMATECH) kwa ajili ya kuzalisha mashine hizo kwa wingi na kuzisambaza nchini kote.
“Hii inaleta matumaini makubwa kwamba wakulima wengi wataweza kumudu teknolojia hiyo,” amesema.
Amesema Mpango wa Taifa wa kuhakikisha kilimo kinachangia angalau asilimia 10 ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2030 unahitaji zana rahisi kama Rafiki Planter.
Hivyo ujio wa mashine hiyo ni ushahidi kwamba kwa uwekezaji sahihi kwenye ubunifu wa ndani, Tanzania inaweza kujitegemea kwenye mapinduzi ya kilimo.
“Tumeweza kutengeneza mashine moja, lakini haitoshi. Tunaomba serikali itusaidie kuzalisha mashine nyingi zaidi ili ziwafikie wakulima kwa wingi. Tukiwezeshwa, tuko tayari kwenda mbali zaidi – si kwa ndoto, bali kwa vitendo,” amesema.
Kwa sasa, timu hiyo ya wabunifu tayari ipo kwenye hatua za mwisho za kutengeneza toleo kubwa la mashine hiyo litakalokuwa na injini ya cc 300, yenye uwezo wa kulima hadi ekari 50 kwa siku – hatua inayokuza zaidi azma ya Tanzania kuwa Taifa la kilimo chenye tija.