Na Lucy Ngowi
ARUSHA: WATAALAMU kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ( SUA), mkoani Morogoro wametoa elimu kwa wafugaji wa Mkoa wa Arusha kuhusu mbinu bora za kudhibiti homa ya kiwele,
Pia namna ya kukabiliana na changamoto ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.

Mhadhiri kutoka SUA ambaye pia ni mtafiti katika Mradi wa NANO COM, Dkt. Shedrack Kitimu amesema chanzo kikuu cha Usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA), ni matumizi mabaya ya dawa kwa binadamu na wanyama.
Vile vile matumizi ya kupita kiasi, kutokumaliza dozi, na matumizi bila ushauri wa kitaalamu ni miongoni mwa sababu zinazochochea usugu huo.
Amesema baadhi ya wafugaji hutumia dawa zisizo na ubora au zilizokwisha muda wake wa matumizi, huku wengine wakitumia dawa kwa ajili ya kukuza wanyama badala ya matibabu.

Pia amesema usafi hafifu, ukosefu wa uchunguzi sahihi wa magonjwa, na ulaji wa mazao ya mifugo bila kuzingatia muda vinachangia tatizo hilo kuongezeka.
“Uchafuzi wa mazingira kwa kutupa mabaki ya dawa kiholela pia huchochea kuenea kwa vimelea sugu,” amesema.
Naye Daktari wa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Dkt. Charles Msigwa amesema zaidi ya asilimia 60 ya wafugaji katika eneo hilo wanafuga ng’ombe wa maziwa, huku changamoto ya homa ya kiwele imekuwa tatizo sugu.
Amesema mafunzo hayo yamewasaidia wafugaji kuelewa umuhimu wa kutunza kumbukumbu za matibabu na matumizi sahihi ya dawa.
Kwa upande wake, Mkazi wa Arusha Martina Mushi, amesema baadhi ya wafugaji hukatisha matibabu ya mifugo ili waendelee na biashara ya maziwa au hutumia dawa zisizofaa, jambo linalochangia usugu wa vimelea.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sivat Agribusiness Ltd. Lopeny Tajiri amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua dalili za UVIDA na namna ya kuwashauri wafugaji katika kudhibiti homa ya kiwele.
Amesema kampuni yao imepata maarifa yatakayowasaidia kuboresha huduma wanazotoa.
Mradi wa NANO COM unatekelezwa na SUA kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali katika mikoa ya Arusha, Tanga, Iringa, Mbeya na Njombe.
Mradi huo unalenga kuboresha afya ya mifugo, usalama wa maziwa, na kuimarisha uelewa kuhusu UVIDA kwa kutafuta tiba mbadala na kusambaza elimu kwa wadau wa sekta ya mifugo.
UVIDA umeendelea kuwa changamoto kwa afya ya mifugo na usalama wa maziwa nchini, hali inayohitaji hatua za pamoja kutoka kwa wadau wa sekta ya mifugo na afya.
Wafugaji 50 walishiriki kwenye mafunzo hayo, wanawake wakiwa 18 Sawa na asilimia 32.