Na Lucy Ngowi
MAKAMU wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewahimiza watendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu katika masuala ya masoko, huku wakilenga kuvutia uwekezaji zaidi.
Dkt. Nchimbi amezungumza hayo leo, Februari 13, 2026, jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa DSE ameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kutafuta mitaji, ili kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, yenye lengo la kufikia uchumi wa Dola za Marekani Trilioni Moja ifikapo mwaka 2050.

Soko la Hisa la Dar es Salaam ni taasisi ya kimkakati ya taifa inayowezesha ukusanyaji na usimamizi wa mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya kufadhili maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
DSE ni jukwaa rasmi linalowawezesha wawekezaji wa ndani na wa kimataifa kufanya biashara ya hisa, hati fungani, na bidhaa nyingine za kifedha katika mazingira yenye uwazi na utawala bora.
Thamani ya jumla ya soko la hisa la Dar es Salaam ni Sh. Trilioni 31.9, ikiwa na jumla ya wawekezaji waliosajiliwa 779,000.
Soko la Hisa la Dar es Salaam ni mwanachama wa Masoko ya Hisa ya Dunia, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).








