Na Lucy Ngowi
MBEYA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imeanzisha programu maalum ya uanagenzi kupitia ofisi yake, inayolenga kuwapatia vijana wa Kitanzania ujuzi wa kazi bila kujali kiwango chao cha elimu.
Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Vijana yanayoendelea mkoani Mbeya, Majaliwa amesema programu hiyo inalenga vijana wote, hususan walioko katika mazingira magumu, ili kuwawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Amesema vijana wote wana nafasi ya kushiriki kwenye mpango huo ambapo serikali inawalipia ada kwa miezi sita wanapokuwa vyuoni, na baada ya kuhitimu wanaweza kujiajiri, kuajiri wengine au kuanzisha vikundi vya uzalishaji mali.

Vijana hao wanapatiwa mafunzo ya stadi mbalimbali zinazochochea uchumi na ajira, ikiwemo ufundi wa magari, umeme, kompyuta, uchomeleaji, usindikaji na ufungashaji wa vyakula, ususi, urembo na ushonaji.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, tangu kuanzishwa kwa programu hiyo mwaka 2022 hadi 2025, jumla ya vijana 77,228 wamepatiwa mafunzo katika vyuo mbalimbali nchini.
Majaliwa amesema maadhimisho ya Wiki ya Vijana ni sehemu ya Siku ya Kimataifa ya Vijana inayotambuliwa duniani kote. Lengo lake ni kutoa fursa kwa vijana kujadili mafanikio, changamoto na nafasi yao katika kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia.
Aliwahimiza vijana kuitumia siku hiyo kueleza changamoto wanazokabiliana nazo ili serikali iweze kuzifanyia kazi kwa ufanisi.
Pia amesema Serikali imefanya maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2017 na sasa inatekeleza sera mpya ya mwaka 2024, inayolenga kuboresha maisha ya vijana kwa kushirikiana nao pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Vile vile imeimarisha programu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na kutoa elimu ya ujuzi bila malipo. Kwa upande wa elimu ya juu, serikali hutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, huku vyuo vya elimu ya kati na ufundi stadi vikiimarishwa kwa lengo la kuwaandaa vijana kuingia kwenye soko la ajira kwa ufanisi zaidi.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amesema maadhimisho ya kila mwaka ya Wiki ya Vijana ni jukwaa la kuwaunganisha wadau wa maendeleo kutathmini mchango wa vijana katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Ameongeza kuwa ni fursa pia ya kuwaenzi waasisi wa taifa, akiwemo Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, waliokuwa katika umri wa ujana walipokuwa wakiongoza harakati za ukombozi wa Afrika.